Fahamu vitu 6 kijana anafaa kuwa navyo pindi anapofikisha miaka 25 - Alinur Mohamed

Kulingana na mwanasiasa huyo, kijana wa miaka 25 anafaa kuwa na angalau shilingi milioni moja pesa za Kenya.

Muhtasari

• Kando na milioni moja, kijana wa miaka 25 anafaa kumiliki simu ya kidijitali, akaunti ya benki inayofanya, kitambulisho cha kitaifa miongoni mwa vingine.

Mwanasiasa Alinur Mohamed
Mwanasiasa Alinur Mohamed
Image: Alinur Mohammed//Facebook

Mwanasiasa Alnur Mohamed amezua gumzo mitandaoni baada ya kuachia orodha ya vitu ambavyo mtu anafaa kuwa navyo pindi tu anapofikisha umri wa miaka 25.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, mwanasiasa huyo wa Nairobi aliwaacha wengi katika mjadala mkali kwa kusema kwamba mtu anapofikisha miaka 25 maisha mwake, ni sharti awe na angalau vitu vitano ikiwemo kuwa na pesa milioni moja za Kenya kwenye akaunti yake.

“Katika umri wa miaka 25, ni lazima uwe na pasipoti, leseni ya kuendesha gari, kitambulisho cha kitaifa, akaunti ya benki yenye inafanya kazi, simu ya kidijitali na angalau shilingi milioni moja ikiwa kiwango cha chini kabisa,” Alinur Mohamed aliandika.

Hili lilikaribisha maoni kinzani kutoka kwa wafuasi wake wengi ambao baadhi walionekana kukubaliana naye huku wengi wakipinga dhana hiyo.

Wale waliopinga walisema kuwa kauli kama hizo ndizo zinawafanya vijana kujihisi chini ya shinikizo pindi wanapofika umri huo pasi na vyote hivyo. Mwisho wa siku kutokana na shinikizo la kuogopa kuitwa mtu aliyefeli kimaisha, wengi huishia kutumia njia za mkato ili kufanikisha kupata vitu hivyo na hivyo kuhatarisha maisha na hata wengine kupoteza maisha katika visa visivyoleta tija maishani.

Wengine pia walizua utani kuwa kitu ambacho wanaweza kuwa nacho pasi na masharti mengi katika umri huo ni kitambulisho cha kitaifa na labda simu ya kidijitali almaarufu Smartphone.

“Si kila mtu ana bahati kama yako maishani,” Mwanablogu Abraham Mutai alimwambia.

“Mimi nina kitambulisho cha kitaifa pekee, langu jicho,” mtangazaji Hassan Ali alitania.

“Mtoto wa kitajiri huwezi elewa maisha ya jamaa wa mtaani. Akaunti ya benki unataka niweke Sukuma wiki ama nguo,” mwingine kwa jina Ngunjiri Ole Muchiri alisema.

“Niko karibu miaka 30 sasa na vitu pekee ninavyomiliki kutokana na ulichotaja hapo juu ni, simu janja na kitambulisho cha taifa...nataka kuamini kuwa nina kitambulisho kwa sababu ni lazima vinginevyo nina shaka ningekuwa nacho. Maisha yetu ni tofauti kabisa kwa hivyo usizungumze takataka wakati ujao,” Hamadi Muaindo Jr alimzomea vikali.