"Hatujaolewa na mtu!" - Gavana wa Nyeri aapa kuongoza Mt Kenya kuondoka UDA

Alisema kwamab waliona kitu katika uteuzi wa wabunge wa EALA bungeni na kudokeza huenda watu wa eneo hilo wakaondoka chama tawala cha UDA.

Muhtasari

• Tungependa kusema bado ni mapema katika hii harusi lakini dalili ya mvua ni mawingu, tukae macho - Kahiga alisema.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga atishia kuongoza Mt Kenya kuondoka UDA
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga atishia kuongoza Mt Kenya kuondoka UDA
Image: Facebook

Gavana wa Nyeri Mutahi Kagiha ambaye alitetea kiti chake kupitia tikiti ya chama cha UDA kwa mara ya kwanza amezungumzia jinsi mchakato wa uteuzi wa Wabunge wa kuwakilisha Kenya katika bunge la Ukanda wa Afrika Mashariki, EALA ulivyofanywa mwishoni mwa wiki hii katika bunge la kitaifa.

Kahiga ambaye ni mwandani wa rais William Ruto alionekana kutofurahishwa na jambo hilo baada ya kutoa matamshi ya kudokeza kuwa ukanda wa Mlima Kenya ulidhulumiwa.

Bila woga, gavana huyo alidokeza huenda akaongoza mamia ya viongozi wa eneo hilo kuondoka katika chama cha UDA na mrengo wa Kenya Kwanza ukiongozwa na rais Ruto katika kile alisisitiza kuwa watu wa mlima Kenya hawajaolewa na mtu.

“Kuna jambo lingine ambalo ningetaka kusema, jambo ambalo linahusu siasa za kitaifa. Tulifuatilia kwa undani kabisa na tukaona mambo yaliyokuwa katika bunge wakati wa uchaguzi wa wabunge wa EALA. Tuliona mambo na tungetaka tuseme sasa kwamba hii safari tutaandamana tukiwa pamoja, au tunaweza pia kusema kama hatutakikani twende pamoja, sisi hatujaolewa na mtu yeyote ambaye anaweza fikiria kuna wakati atatupeleka leo hivi keshi vile,” Gavana Kahiga alizungumza wakati wa kuapishwa kwa mawaziri wa kaunti ya Nyeri.

“Sisi tulitazama jana na tukaona kwamba kuna watu ambao walijaribu kutuzunguluka. Wanajaribu kuleta ukora katika siasa, tuliapa kufanya kazi pamoja lakini baadhi ya watu wanapinga jambo hilo, ndiyo maana tulimchagua Kanini Kega, na tukajitolea kufanya kazi pamoja na tutaendelea kuchagua watoto wetu kama tunaletewa mchezo kama huu. Tungependa kusema bado ni mapema katika hii harusi lakini dalili ya mvua ni mawingu, tukae macho," Kahiga aliongeza.

Matamshi haya ya gavana yaliibua mgawanyiko mkubwa kwenye mtandao wa Twitter baadhi wakiibua kumbukumbu kuwa hivyo ndivyo chana cha Jubilee kilizama majini baada ya migawanyiko kama hii kuanza kuonekana mapema mwaka 2018.