Vijana wenye hasira wamtafuta jambazi aliyeua rafiki yao na kumpiga kitutu

Kennedy Mwangi alishambuliwa na genge la majambazi lakini kabla hajafa hospitalini, alitaja jina la mmoja wa majambazi hao.

Muhtasari

• Walimfuatilia mshukiwa huyo kwa siku kadhaa na hatimaye kumvuta nje ya maficho yake. Alipigwa kikatili.

Crime Scene

Kundi la wanaume mjini Naivasha limewasaka majangili waliomuua rafiki yao na kulipa kisasi kwa niaba yake.

Marehemu alishambuliwa na genge hilo la wezi mwishoni mwa mwezi Oktoba mjini Naivasha alipokuwa akirejea katika makaazi yake. Majambazi hao walimjeruhi vibaya na kumuaacha ajifie mwenyewe ambapo marafiki wake walifika kwa muda na kumpeleka hospitalini.

“Alijitahidi na watesaji wake kujinasua kutoka kwa mshiko wao thabiti shingoni mwake. Alijeruhiwa vibaya sana, baada ya saa chache afariki dunia. Alikuwa amemtambua mmoja wa washambuliaji hao na kabla hajafa, alitaja jina lake kwa marafiki zake,” jarida la Nation liliripoti.

Baada ya kufariki kwake, marafiki zake waliojawa na ghadhabu na uchungu mno walishindwa kujizuia na hapo ndio waliamua kukinukisha mtaa mzima kwa kuwatafuta majambazi hao ili kulipa kisasi kwa niaba ya rafiki yao marehemu Kennedy Mwangi.

“Walimfuatilia mshukiwa huyo kwa siku kadhaa na hatimaye kumvuta nje ya maficho yake. Alipigwa kikatili, lakini polisi walifika kwa wakati na kumuokoa muuaji aliyepoteza fahamu kutoka kwa vijana waliokuwa na hasira.”

Walilipiza kisasi na kumshtumu kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu na kushambulia watu "aliokuwa akifahamiana nao".

Baada ya kuokolewa na polisi, mwizi huyo mmoja anasubiriwa kupona kabla ya kufunguliwa mashtaka ya uhalifu na mauaji huku msako dhidi ya wenzako walioshirikiana kumuua jamaa huyo ukiendelea.