Sudi na Alai watupiana lawana Twitter kufuatia chapisho la gazeti

Chapisho lilifichua mwanasiasa mmoja aliyetumia ukaribu wake na viongozi wa juu Kenya Kwanza kuwalaghai wenzake.

Muhtasari

• Mwanaume huyo alitumia ukaribu wake na mwanasiasa wa ngazi ya juu ndani ya Kenya Kwanza kuwadanganya waathiriwa - sehemu ya jarida hilo ilisoma.

Alai na Sudi watukanana mitandaoni
Alai na Sudi watukanana mitandaoni
Image: Facebook

Mbunge wa Kapsabet Oscar Sudi na diwani wa Kileleshwa Robert Alai wameendelea kushambuliana kwa maneno yasiyo na soni kwenye mtandao wa Twitter baada ya Alai kuibua madai kuwa Sudi aliwalaghai wanasiasa kadhaa kwa lengo la kuwaahidi kazi katika serikali ya rais William Ruto.

Sakata lilianza baada ya  Robert Alai kupakia sehemu ya gazeti moja la humu nchini lililokuwa limedokeza kuwa kuna mwanasiasa mmoja kutoka ukanda wa Bonde la Ufa ambaye alitumia ukaribu wake na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu katika serikali ya Kenya Kwanza kuwarubuni wenzake waliopoteza kura kuwa atawahakikishia nafasi za kazi ndani ya serikali.

“Mwanasiasa mzungumzaji sana kutoka Bonde la Ufa amepoteza uaminifu wake kutoka kwa ofisi kuu nchini baada ya shtuma za ulaghai. Mwanasiasa huyo alitumia nafasi yake na kuwalaghai mamilioni ya pesa wanasiasa ambao walikuwa wanamezea mate nyadhifa mbalimbali katika serikali. Mwanaume huyo alitumia ukaribu wake na mwanasiasa wa ngazi ya juu ndani ya Kenya Kwanza kuwadanganya waathiriwa kuwa angewahakikishia kuteuliwa katika nyadhifa za kumezewa mate serikalini,” sehemu ya jarida hilo ilisoma.

Isitoshe, Alai alienda mbele na kunukuu jairda hilo akilitaja jina la Sudi kuwa hakuna mwingine bali ni yeye ila akasema kuwa angepata uhakika zaidi baada ya kulizamia hilo.

“Huyu ni nani? Si ni Sudi tu ambaye huenda alilaghai watu. Acha niulizie watu wangu walioko ikulu, hili litajulikana ifikapo kesho,” Alai aliandika.

Sudi akionekana kujawa na hasira alibwatuka na kumzomea Alai huku akijiweka mbali na madai hayo na kusema kuwa yeyote anayedhani ni yeye aliyewarubuni watu basi yupo huru kupiga ripoti polisi.

“Kwani ni nini? Tafahdali piga ripoti kwa polisi  iliyokaribu nawe, mnafikiria mimi ni mtu wa bei ya chini hivyo? Siwezi kunywea kwa madai yako yasiyo na mashiko kama yale ambayo umetumia kwa watu mpaka wakakuhakikishia kazi ya kupata mshahara. Huwezi kunilaghai rafiki yangu, kamwe!” Sudi alitupa bomu la moto mdomoni mwa Alai.