Machakos: Mwanamke afukuzwa kwa kutumia uchawi kuzuia mvua kunyesha

Wanakijiji walimtuhumu kwa kuficha kiungo cha mwili wa mwanaume ambacho anakitumia kufanya ushirikina kuzuia mvua.

Muhtasari

• Tukio hili linalosimulika kama filamu ya kustaajabisha lilitokea baada ya wanakijiji kujumuika na kumhamisha mwanamke huyo kwa nguvu.

Vitu vya kishirikina
Vitu vya kishirikina
Image: Hisani

Mwanamke mmoja kutoka kaunti ya Machakos Jumanne alifurushwa nyumbani kwake na majirani waliojawa na ghadhabu baada ya kudaiwa kutuia ushirikina ili kuzuia mvua zisinyeshe kaunti hiyo.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa na Citizen Digital, mwanamke huyo wa miaka 48 mkaazi wa Yatta kaunti ya Machakos alivamiwa na majirani waliomshrutisha kuhama nyumbani kwake kwa kile walisema kuwa ndiye chanzo cha mvua kutonyesha eneo hilo kwa miezi kadhaa sasa.

“Wanakijiji walivamia nyumba yake siku ya Jumanne, na kubomoa paa la nyumba yake na kuondoa mali zake zote. Katika shutuma ambazo zilisikika kama filamu ya kutisha, majirani hao walidai kuwa mwanamke huyo alikuwa na kiungo cha uzazi cha mwanaume, ambacho inadaiwa anakitoa asubuhi ili kuzuia mvua kunyesha,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Iliwalazimu maafisa wa kutuliza ghasia kufika katika kijiji hicho ili kutuliza hasira za wanakijiji waliokuwa wamejawa na ghadhabu.

Walisema kuwa walimchinja mbuzi na kumlazimisha mwanamke huyo kunywa damu kama moja ya njia za mila kumtakasa.

Polisi walisema kuwa mwanamke huyo alilazimika kuamishwa kwenye kituo cha polisi cha hapo karibu kutokana na kuwa na mtoto mtahiniwa wa darasa la nane katika shule ya eneo hilo ambaye anatarajia kufanya mtihani wa kitaifa wiki moja ijayo.

Eneo la Ukambani kwa muda mrefu limekuwa likishuhudia uhaba wa mvua na kukumbwa na kiangazi kwa muda mrefu ambapo mvua kunyesha katika eneo hilo ni nadra sana.