Gavana Wanga atembelea familia ya mtahiniwa wa KCSE aliyefariki akijifungua

Gavana Wanga alionekana akiwa amempakata mikononi mtoto huyo wa siku moja, katika picha ambazo ni za kutia huruma mno.

Muhtasari

• Gavana alitoa amri kwa idara husika kufanya uchunguzi huru kila moja na kutoa majibu yake ambapo hatua faafu zitachukuliwa baada ya hapo.

• Velma Anita Ochieng alifariki baada ya kusemekana kupata matatizo baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji huko Homabay.

Gavana wa Homabay Gladys Wanga akiwa amempakata mikononi mtoto wa siku moja wa mwanafunzi huyo.
Gavana wa Homabay Gladys Wanga akiwa amempakata mikononi mtoto wa siku moja wa mwanafunzi huyo.
Image: Facebook

Gavana wa Homabay Gladys Wanga Jumanne asubuhi alitembelea na kuifariji familia ya Velma Anita Ochieng, mtahiniwa wa kidato cha nne aliyefariki akijifungua mtoto siku ya Jumatatu.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19 aliripotiwa kufariki kutokana na matatizo ya kiafya yaliyojiri baada ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua mtoto.

Mtoto alinusurika lakini mamake alifariki dunia, siku chache tu kabla ya kung’oa nanga kwa mitihani ya kitaifa, KCSE.

Wanga alionekana akiwa amempakata mtoto huyo wa siku moja mikononi katika picha ya kutia huruma na kusema kwamba ametoa amri kwa idara husika katika kaunti hiyo kuanzisha uchunguzi na kila moja kutoa majibu yake huru kuhusu kile kilichojiri mpaka mwanafunzi huyo akapoteza maisha kabla hata ya kumpakata mtoto wake.

“Asubuhi ya leo, nimetembelea na kufariji familia ya Velma Anita Ochieng, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 19 ambaye alikabiliwa na matatizo ya baada ya kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homabay. Nimeagiza Idara ya Afya ya Kaunti na Kamati ya Huduma za Tiba ya Bodi ya Hospitali ya Rufaa kufanya uchunguzi huru kivyake kuhusu hali iliyosababisha kupoteza maisha ya Velma. Hatua na vitendo vya lazima vitafuata,” gavana Wanga alisema.

Velma Ochieng, ambaye ni mtahiniwa wa KCSE katika Shule ya Sekondari ya Nyajanja iliyoko Kochia, Rangwe, aliaga dunia Jumatatu muda mfupi baada ya kujifungua mtoto mvulana kwa ufanisi.

Alikuwa amelazwa katika kituo hicho Jumamosi jioni baada ya kupata matatizo ya ujauzito kabla ya wakati.