Joho apakia picha akiwa ughaibuni, watu wataka kujua kama atakuwa Maandamano

Kwa muda mrefu Joho amekuwa mwandani wa Odinga na kila mtu alishangaa mbona hayupo nchini kwa ajili ya maandamano ya Jumatano.

Muhtasari

• Jumatatu asubuhi, naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera alitangaza kujiuzulu siku chache baada ya kamishna Justus Nyang’aya pia kujiuzulu.

Naibu kiongozi wa chama cha ODM Wycliff Oparanya, mgombea urais wa ODM Raila Odinga na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho wakati wa Baraza la Kitaifa la Uongozi katika Bomas Of Kenya mnamo Februari 25,2022.
Image: ENOS TECHE

Baadhi ya Wakenya watumizi wa mtandao wa Instagram wamemvaa aliyekuwa gavana wa Mombasa Hassan Joho baada ya kupakia picha akiwa ughaibuni kujivinjari.

Joho alipakia picha akiwa katika nchi moja ughaibuni na kusema kuwa kulikuwa na baridi kali, lakini mashabiki wake hawakutaka kusikia hilo bali walitaka kujua ni kwa nini hayuko humu nchini kujiandaa kwa maandamano yatakayoongozwa na Raila Odinga katika uwanja wa Kamkunji kupinga hatua ya serikali kuwasimamisha kazi makamishna wane wa IEBC.

Joho kwa muda mrefu amejulikana kuwa mwandani wa kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga na wengi walitaka kujua iwapo ana mpango wowote wa kuhudhuria mkutano huo wa kuandaa maandamano au la.

Wengine walimtania kuwa yeye ndiye alisemekana kuwa na firimbi ambazo zitatumika katika maandamano hayo hali ya kuwa bado yuko ughaibuni.

Maandamano iko kuanza na wewe bado unacheza na mascooters huko?? Junet anasema wewe ndio uko na firimbi😂😂😂” Its Bonham alimuuliza.

Ikumbukwe wakati wa kampeni za Azimio, Odinga aliweka wazi kuwqa angeshinda angemteua Joho moja kwa moja kama waziri wa ardhi. Wengi walitumia hili pia kumkejeli huku wakimtaja kuwa ni waziri hewa wa ardhi.

“CS wa ardhi sasa wewe pia utakuwa kwa maandamano?” mwingine alimuuliza.

Odinga aliweka wazi kuwa Jumatano wiki hii yeye na wafuasi wake watakongamana katika uwanja wa kamkunji jijini Nairobi ili kuzindua maandamano ya kitaifa kwa ajili ya kuwatetea makamishna wane wa IEBC ambao wanaelekea kupoteza kazi yao baada ya kamati ya JLAC kupendekeza wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi zaidi dhidi yao.

Jumatatu asubuhi, naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera alitangaza kujiuzulu siku chache baada ya kamishna Justus Nyang’aya pia kujiuzulu.

Wajuzi wa masuala ya kisiasa walisema hatua hii huenda ikalemaza pakubwa maandamano ya Odinga ambayo yanatarajiwa kufanyika siku mbili zijazo.