Betty Bayo ashaolewa, na wewe tafuta mke mwingine - Ng'ang'a amshauri Kanyari

Victor Kanyari aliachwa na Betty Bayo baada ya Jicho Pevu kufichua maovu yake kwa waumini.

Muhtasari

• "Nilikuwa nakuambia, si mke alienda, kwa hivyo tafuta mwingine pia nawe” Ng’ang’a aitania.

• Victor Kanyari aliachwa na Betty Bayo baada ya Jicho Pevu kufichua maovu yake kwa waumini.

Ng'ang'a amshauri Kanyari aoe tena
Ng'ang'a amshauri Kanyari aoe tena
Image: Maktaba

Mwanzilishi wa Neno Evangelism Mchungaji James Ng’ang’a amemwambia Nabii Victor Kanyari aendelee na kutafuta mke.

 

Wikendi iliyopita mchungaji James Ng’ang’a alikuwa na mkusanyiko mkubwa wa injili katika uwanja wa Jacaranda jijini Nairobi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya watu ambapo baadae alishangaa kumuona mchungaji mwenza, Victor Kanyari akiwa miongoni mwa wale waliohudhuria.

 Kwa mshangao, Ng’ang’a alimuita Kanyari kujongea mbele kwenye madhabahu ili kumsalimia na pia kuwasalimia waumini.

Pia, mchungaji huyo mwenye utashi mwingi alitumia fursa hiyo kumdadavulia Kanyari ushauri wa kumtaka atafute mke mwingine na kuoa.

Ng’ang’a kwa mzaha alimwambia Kanyari kuwa aliyekuwa mke wake, mwinjilisti Betty Bayo tayari ameshasonga mbele na maisha na sasa ni mume wa mtu na hivyo kuna haja kwa Kanyari pia kuchukua mkondo huo na kutafuta mke mwingine.

“Kwani Kanyari uko hapa? Huu mkusanyiko wa injili umehudhuriwa, Mtumishi wa Mungu njoo mbele unisalimie, na umepungua uzito mzee. Nilikuwa nakuambia, si mke alienda, kwa hivyo tafuta mwingine pia nawe” Ng’ang’a aitania.

Kanyari akitabasamu alichukua kipaza sauti na kusema alihudhuria ibada hiyo kwa vile Mchungaji Ng’ang’a alikuwa kama babake wa kiroho.

“Nilikuwa nimejificha nyuma  pale kwa sababu ninaogopa, lakini namshukuru Mungu."

Mchungaji Ng’ang’a aliendelea kueleza kuwa Mchungaji Kanyari na wahubiri wengine wanaokuja wanapenda kufanya makosa lakini anawarekebisha.

"Makosa mawili hayawezi kufanya haki. Nilipofika Nairobi nilikuwa nikihubiri katika kanisa la Mchungaji Kanyari huko Kawangware. Niliona baadhi ya mambo hayakuwa sawa na nikamwambia.”

Miezi michache iliyopita, Kanyari aliiambia blogu moja kuwa alikuwa tayari kuunganishwa na mwanamke ‘mzuri’ anayevutiwa. Alisema hatatafuta sura ingawa atamwomba Mungu amwongoze katika kuchagua.

Bayo alifunga ndoa ya kitamaduni miezi kadhaa iliyopita na mwanaume mmoja ambaye alisema alimkubali na wanawe na sasa ni mtu mwenye furaha kwenye ndoa.

Bayo na Kanyari walitengana miaka kadhaa iliyopita baada ya Jicho Pevu kutumbua maovu ya mchungaji Kanyari jinsi alivyokuwa akiwarubuni waumini kwa kuwashrutisha kutoa sadaka ya 310.