Tushirikiane kumsaidia mtoto Sagini-Sonko kwa viongozi wa Kisii

Sonko alisema kuwa havutiwi na kiti chochote cha kisiasa kwa sasa kwa hivyo sio kikwazo cha kisiasa.

Muhtasari
  • "Sigombei kiti chochote Kisii, muda wa kampeni umekwisha. Mimi ni mtu tu wa kusaidia watu," alisema
  • Alisema amejitolea kusaidia kesi ya kusikitisha ya mtoto Sagini kwa sababu ya historia yake ya kusaidia watu
Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Image: Facebook//Mike Sonko

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko amesema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Kaunti ya Kisii wanaomzuia kumsaidia mtoto Sagini.

Sonko alisema kuwa havutiwi na kiti chochote cha kisiasa kwa sasa kwa hivyo sio kikwazo cha kisiasa.

"Sigombei kiti chochote Kisii, muda wa kampeni umekwisha. Mimi ni mtu tu wa kusaidia watu," alisema.

Alisema amejitolea kusaidia kesi ya kusikitisha ya mtoto Sagini kwa sababu ya historia yake ya kusaidia watu.

"Kikosi cha Sonko Recuse kimekuwa na visa vingi vikali kama vile vya mtoto Stanley kutoka Kericho, msichana aliyekuwa na uvimbe kwenye ubongo na tukampeleka hadi. India, mtoto Kayla ambaye tulimpeleka India na upasuaji ulifanikiwa," alisema.

Sonko alisema hata katika kesi ya mtoto aliyepigwa risasi na magaidi wa Al Shabaab waliingilia kati na mtoto huyo bado yuko hai miaka 10 baadaye.

"Hatuwezi kuwa tumekuwa tukicheza PR na mtoto wa mtu kwa miaka kumi," alisema.

Aliwaomba viongozi wa Kisii kushirikiana naye na kufanya kazi naye ili kumsaidia mtoto Sagini na dadake.

"Tunamheshimu Gavana wa Kisii na kila mtu katika Kisii kwa hivyo tafadhali, tushirikiane kumsaidia mtoto Sagini na kumtoa mtoto Sagini na kumpatia usaidizi mkubwa wa kimatibabu," alisema.

Aliwataka viongozi hao kuweka kando tofauti za kisiasa badala yake wasaidie watoto hao.