MP Peter Kaluma aunga KeMU mkono kupiga marufuku uvaaji 'mbaya', watu wamshambulia

"Tunafundisha viongozi katika nyanja mbalimbali, sio makahaba!” Kaluma aliandika.

Muhtasari

•Kaluma alisema kuwa sheria hizo zinafaa kukumbatiwa na vyuo vikuu vyote pamoja na taasisi za masomo nchini.

• KeMU walitoa orodha ndefu ya sheria mpya kuhusu uvaaji wa wanafunzi wao ambazo zinaatanza kutekelezwa mara moja.

Mbunge Kaluma aunga mkono chuo cha KeMU kupiga marufuku uvaaji usio na stara.
Mbunge Kaluma aunga mkono chuo cha KeMU kupiga marufuku uvaaji usio na stara.
Image: Twitter,

Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma amekuwa wa hivi karibuni kukaribisha hatua ya chuo cha Kenya Methodist kupiga marufuku baadhi ya mavazi na muonekana kwa wanafunzi wa chuo hicho.

Mwishoni mwa wiki jana, barua kutoka kwa ofisi ya usimamizi wa wanafunzi wa chuo cha KeMU ilisambaa mitandaoni ikionesha baadhi ya maagizo mapya kuhusu uvaaji na muonekano wa mwanafunzi yeyote kabla ya kutia guu ndani ya malango ya chuo hicho.

Baadhi ya sheria hizo mpya ambazo zinaanza kufanya kazi mara moja ni wanafunzi kutosuka nywele kwa mtindo wa kirasta, nywele zilizopakwa rangi, vipini vya masikioni, uvaaji wa shati ambazo hazijasokotwa vizuri ndani ya suruali ndefu, na uvaaji wa kofia vyote ni marufuku kwa watoto wa kiume.

Kwa upande wa watoto wa kike, ni marufuku kuvaa blausi fupi zinazoonesha kitovu, migongo wazi, sketi ambazo mipasuo yao inazidi juu ya goti, nguo zinazonata kwa miili, nguo zenye uwezo wa kuonesha vya ndani na sketi fupi.

Kaluma ametoa kongole kwa uongozi wa chuo hicho kwa kuchukua hatua hii ambayo aliitaja kama ya kurudisha heshima na ustaarabu katika vyuo vikuu.

Mbunge huyo alisema kuwa hatua hiyo itahakiisha vyuo vinatoa watu wenye maadili mema ambao wana uwezo wa kuwa viongozi katika jamii na wala si watu wa kujitembeza na kujiuza.

“Hili linapaswa kutekelezwa na Vyuo Vikuu vyote na taasisi za masomo. Tunafundisha viongozi katika nyanja mbalimbali, sio makahaba!” Kaluma aliandika kwenye Twitter.

Maoni yake yalivutia hisia mseto, baadhi wakisema kuwa enzi za sasa si kama za zamani ambapo watu walikuwa wanavaa kwa masharti fulani.

Hata hivyo, kuna owaliomuunga mkono wakisema kuwa maadili yametokomea katika jamii nyingi kutokana na uvaaji usio wa kiheshima.

“Wazee wa kizamani kubali kuzeeka kwa kipooole, hii labda ifanyika kwa vyuo vyenu si kwa kizazi cha sasa,” Chepkurui Irene alisema.

“Maadili na uasherati vitakuwepo hadi mwisho. Siku zote kutakuwa na watu wanaounga mkono uasherati na watafanya hivyo hadi Mungu atakapowaangamiza. Hakuna mwanadamu anayeweza kukomesha uasherati ila tu Mungu atafanya wakati utakapofika,” John alisema.