Seneta Boni Khalwale atupa boma la moto Marekani kuhusu LGBTQ

Khalwale alisema kuwa USA ndio imechangia katika watoto wengi wa Kiafrika kupotoka kimaadili.

Muhtasari

• "USA, kaa mbali na watoto wetu. Tafadhali!” Khalwale alisema kwa ukali wake uliopitiliza.

• Nchini kuna mjadala mkali kuhusu LGBTQ kufuatia kifo cha Edwin Chiloba ambaye alikuwa mwanaharakati wa jamii hiyo.

Boni Khalwale, seneta mteule wa Kakamega
Boni Khalwale, seneta mteule wa Kakamega
Image: Facebook//Boni Khalwale

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amekuwa mtu wa hivi karibuni kutia kweney mizani suala la jamii ya LGBTQ nchini Kenya kufuatia kifo cha utatanishi cha aliyekuwa mwnaharakati wa jamii hiyo Edwin Kiprotich Kiprop almaarufu Chioba.

Khalwale aliishtumu vikali ripoti kutoka kwa msemaji wa masuala ya nje wa Marekani Ned Price kwamba serikali ya Marekani iko tayari kutoa usaidizi wa aina yoyote katika kufanikisha uchunguzi wa mauaji ya Chiloba.

Seneta huyo mwenye misimamo mikali alisema kauli kama hiyo kutoka kwa serikali ya Marekani inalenga kutoa msukumo zaidi pamoja na motisha kwa visa vya wapenzi wa jinsia moja nchini, jambo ambalo alisema ni kinyume na tamaduni lakini pia desturi na ustaarabu wa Kiafrika.

Aliitaka Marekani kukaa mbali kabisa na suala hilo kwani Kenya bado mambo ya LGBTQ ni haramu na kuingiliwa na Marekani ni kama kuwapotosha vijana wa Kiafrika.

“Ikiwa serikali za Kiafrika zinatafuta ni nani anayeharibu muundo wa kijamii wa Kiafrika unaoheshimika kwa muda mrefu miongoni mwa vijana wetu, usiangalie zaidi. USA, kaa mbali na watoto wetu. Tafadhali!” Khalwale alisema kwa ukali wake uliopitiliza.

Siku mbili zilizopita, msemaji huyo wa Marekani alinukuliwa na jarida la Washington Blade akisema kuwa Marekani ilikuwa inafuatilia suala la mauaji ya Chiloba kwa ukaribu huku akitaka wahusishwe kama watahitajika kufanya hivyo.

“Tunawaomba na kutarajia Wakenya kufanya uchunguzi wa kina na wa uwazi kuhusu kifo chake," Price, ambaye ni shoga waziwazi, aliambia Washington Blade wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kila siku. "Na kwa kweli ikiwa kuna chochote tunaweza kufanya kusaidia, tuko tayari kufanya hivyo."

Kauli hii ilijiri wakati ambapo Wanasiasa mbalimbali wanaendelea kutoa maoni yao kuhusu suala zima la LGBTQ huku wabunge Oscar Sudi, Mohammed Ali na Mish Mboko wakishtumu vikali jamii hiyo na kusema kwamba Kenya hakuna sheria ya kuhalalisha vitendo kama hivyo ambavyo walivikemea kwa maneno mazito kama nanga.