Bodi ya famasia imeonya dhidi ya uhalali wa vifaa vya DNA vya Ksh 800 nchini Kenya

Bodi hiyo ilisema vifaa hivyo ni feki na havijapewa kibali cha kuuzwa nchini Kenya kama ambavyo baadhi walikuwa wanadai mitandaoni.

Muhtasari

• Wiki jana kulisamabzwa habari mitandaoni kuwa vifaa vya kupima DNA nyumbani vitakuwa vinachuuzwa nchini kwa bei ya rejareja ya Ksh 800.

Kifaa cha kupima DNA nyumbani
Kifaa cha kupima DNA nyumbani
Image: Maktaba

Takribani wiki moja tangu habari ya ujio wa vifaa vya kupima DNA kubaini kama mtoto ni wako zisamabzwe mitandaoni, sasa serikali imezungumzia suala hilo kwa mara ya kwanza.

Vifaa hivyo vya DNA vilisemekana kuwa vitakuja kwa bei nafuu ambayo wengi wa wakenya wenye kipato cha uchumi wa kati wanaweza kumudu kununua na kubaini uhalali wa watoto wanaowalea. Fununu zilisema kuwa vifaa hivyo vitauzwa kwa kati ya shilingi 800 hadi elfu moja na havihitaji utaalamu wowote kwa mtu kuvitumia kwani mtu anaweza kuvinunua na kujifanyia vipimo mwenyewe nyumbani kwake.

Wizara ya afya kupitia bodi ya kusambaza dawa na kudhibiti usambazwaji wa sumu, PPB, iliandika Twitter kuwa vifaa hivyo ni feki na serikali haijatoa kibali chochote kwa vifaa hivyo kuuzwa kwa Wananchi.

“Tumefahamishwa kwamba kuna vifaa visivyoidhinishwa vya kupima DNA nyumbani ambavyo vinapigwa mnada kweney mitandao ya kijamii nchini Kenya. Tafadhali ifahamike kwamba PPB haijaidhinisha rejareja kuuza vifaa hivyo na hivyo kutoa wito kwa umma kuwa macho kwa wauzaji wa rejareja wanaouza vifaa hivi," ilisoma sehemu ya taarifa hiyo iliyotiwa saini na Dk Siyoi, Mkurugenzi Mtendaji wa PPB.

Hata hivyo, habari hizi hazikupokelewa vyema na baadhi ya Wakenya kwenye mtandao wa Twitter ambao walisuta PPB vikali wakiwaambia wabaki kwenye mstari wao wa kudhibiti dawa na sumu wakisema kuwa vifaa hivyo havina uhusiano wowote na majukumu yao kama PPB.

Wengine walisema kuwa PPB ni kama inajaribu kuunga mkono uhanyaji katika ndoa huku wakiwataka wakome na waache Wakenya haswa wanaume wajipatie vifaa hivyo na kujua uhalali wa watoto ambao wanalea katika ndoa.

Wapema wiki hii, mfanyibiashara Mike Sonko alitoa wosia kwa Wakenya kutojaribu kuendea vifaa hivyo katika kile ambacho alisema kuwa ndoa nyingi zitavunjika kwani Wanaume wengi nchini huenda wanalea watoto ambao si wao na ikija kubainika si tu ndoa zitavunjika bali hata visa vya mauaji vitaongezeka kwa kasi kubwa.