"Mlinipa 1% ya kura, mkiendelea kunibagua nitawashtaki kwa Mungu," rais Ruto akiwa Homabay

Ruto alikuwa akizungumza kwa utani akisema kuwa Odinga alipata asilimia kubwa katika ngome zake, kuliko vile yeye alipata Nyanza.

Muhtasari

• Unajua sasa Agwambo huko kwetu hata kwa kina Rigathi Agwambo alipata 25% huko kwetu akapata 28%. Hapa mlinipatia 1% - Ruto.

rais Ruto azua mzaha kwa kura alizopata Homabay
rais Ruto azua mzaha kwa kura alizopata Homabay
Image: Facebook

Ijumaa Januari 13, rais Ruto alianza ziara yake rasmi ya kuzindua mirandi ya kimaendeleo katika mkoa wa Nyanza, ziara ambayo itachukua siku mbili.

Rais aliwashangaza wengi baada ya kutangaza kwamba ziara yake ya kimaendeleo ya kwanza kabisa tangu achukue hatamu kama rais ingeanzia Nyanza – ngome ya mpinzani wake mkubwa, kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Akiwa katika kaunti ya Homa Bay, Ruto alilakiwa kama shujaa na viongozi pamoja na wakaazi wa kaunti hiyo, wakiwemo gavana Gladys Wanga, waziri wa ICT Eliud owalo miongoni mwa watu wengine wengi.

Katika hotuba yake, rais aliibua utani kwa kukumbuka kuwa watu wa kaunti hiyo walimpa kura asilimia moja tu ya kura zote, na watu walipasua vicheko kwa utani huo wa kimzaha.

Ruto kwa vicheko, aliwakumbusha watu wa Homa Bay kuwa alishindwa kuwatongoza kisiasa ili kumpa kura, kinyume na Odinga ambaye alifanikiwa kuwatongoza watu wa ngome za Ruto na kupata angalau asilimia 20 ya kura ikilinganishwa na asilimia moja ambayo yeye alipaka katika ngome za Odinga.

Niliwaambia mnikumbuke jameni. Lakini sasa hata nyinyi mko na maneno. Unajua sasa Agwambo huko kwetu hata kwa kina Rigathi Agwambo alipata 25% huko kwetu akapata 28%. Hapa mlinipatia 1% . Na nilikuwa nimewaambia mkiendelea kunibagua nitawashtaki kwa Mungu nyinyi," rais Ruto alisema kwa umati uliojawa na mbwembwe.

Leo hii Jumamosi, Ruto anatarajiwa kuendelea ziara hiyo katika kaunti zingine kama Siaya, Kisumu na Migori.

Awali, viongozi wa mrengo wa upinzani walikuwa wamesemekana kuwa wangesusia ziara hiyo lakini baadae Odinga aliwarai viongozi wote kuhudhuria ziara ya rais kwani ilikuwa si ya kisiasa bali ni ya kimaendeleo.