Kama mwana mpotevu nimerudi, naomba unipokee - Nick Salat amuomba rais Ruto

Salat alikuwa katibu wa chama cha KANU kabla ya kusimamishwa kazi akisubiri uchunguzi na kutokea mbele ya kamati ya adhabu ya KANU.

Muhtasari

• Salat ambaye amekuwa akimshtumu Ruto hapo awali alionekana kubadili wimbo wake na kumsifu huku akimuomba kumkubali ndani ya serikali.

Nick Salat akisalimiana na Ruto
Nick Salat akisalimiana na Ruto
Image: Facebook

Aliyekuwa katibu wa chama cha KANU Nick Salat hatimaye amepata kambi mpya katika ubavu wa rais William Ruto baada ya kusimamishwa kazi na kufurushwa katika chama hicho kikongwe zaidi nchini.

Salat ambaye enzi akiwa katika chama cha KANU kinachoongozwa na Gideon Moi, alikuwa akimtupia cheche kali Ruto lakini baada ya kimbunga kuvuma upande wake, ameruka upande wa serikali na kuasi mrengo wa Azimio ambao KANU walikuwa moja ya vyama vilivyounda muungano huo.

Salat alimsubiri rais Ruto katika kaunti ya Bomet ambapo alihudhuria ibada ya pamoja ya makanisa mbali mbali na kumpa hakikisho Ruto kuwa atamuunga mkono kwa miaka kumi ijayo bila kurudi nyuma katika chama cha KANU.

“Nataka kukuhakikishia kuwa nitakuunga mkono kwa njia zote. Siwezi kumudu kuwa nje ya serikali, kuwa mbali na wengi. Nimerudi kwenye mkumbo. Kama mwana mpotevu, nataka kusema hadharani kwamba nitakuunga mkono kwa Urais kwa miaka 10 ijayo. Tafadhali nikubali na uniingize katika serikali yako ambayo ni kubwa ya kututosha sote,” Salat alimuomba rais Ruto.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wengi ilimuona mkuu wa baraza la mawaziri Musalia Mudavavi akimtetea Salat huku akimtaja kama kiongozi shupavu ambaye alipoteza miaka 15 katika chama cha KANU.

Mwenyekiti wa KANU Gideon Moi siku kadhaa zilizopita alitangaza kusimamishwa kwa Salat kama katibu kwa muda huku akitarajiwa kufika mbele ya kamati ya adhabu ya chama hicho kujibu madai yaliyoibuliwa dhidi yake.