Mmiliki wa Twitter Elon Musk amedai Instagram huwapa watu msongo wa mawazo

Musk alitetea Twitter na kusema huwa inawapa watu hasira za muda tu ikilinganishwa na Instagram ambayo alidai huwapa watu unyongovu.

Muhtasari

• Baadhi walihisi mkwasi huyo amechimbua vita vya maneno baina yake na mmiliki wa Meta, Mark Zucherburg.

Elon Musk aanzisha vita na Instagram ya Zuckerberg
Elon Musk aanzisha vita na Instagram ya Zuckerberg
Image: Twitter, facebook

Mmiliki wa mtandao wa Twitter Elon Musk ametoa kauli mpya kuhusu mitandao ya kijamii, akilenga kulinganisha madhara ambayo yanaletwa na mitandao mbali mbali.

Kulingana na Musk, mtandao wa Instagram ambao unamilikiwa na wapinzani wake wa Meta ambao pia wanamiliki Facebook, mtandao huo unawafanya watu wanakuwa chini ya shinikizo kupelekea kupata unyongovu na msongo wa mawazo.

Kwa upande mwingine, Musk amesema kuwa mtandao wa Twitter unawafanya watu wanajawa na hasira zisizo na maana, huku akiwauliza wafuasi wake kutoa kauli yao kuwa ni mtandao upi bora kwa mtu kutumia pasi na kupata madhara yoyote.

“Instagram huwafanya watu kuwa na huzuni na Twitter huwakasirisha watu. Ambayo ni bora zaidi ni ipi?” Elon Musk aliuliza.

Musk ambaye mwaka jana alifanikiwa kununua mtandao huo wa Twitter kwa upande wake alisema kuwa huwa anapata furaha yake katika kutweet kuhusu mambo tofauti kwenye mtandao huo ambao alisema huwafanya watu wengi kujawa na hasira.

Baadhi ya watu walitoa maoni yao kuhusu kauli hiyo ya Musk, wakijaribu kutoa tofauti kati ya Instagram na Twitter.

“Twitter hunipa habari na hunifahamisha. Instagram inanionyesha picha za watu ambao sijali chochote na sasa wanajaribu kuwa tik tok. Nitachukua twitter,” TJ Moe alisema.

“Twitter inafurahisha isipokuwa akaunti yako idhibitiwa. Zaidi ya hayo, mjadala wa wazi ni jambo zuri. Ningechagua Twitter badala ya Instagram siku yoyote!” mwingine alisema.

“Instagram huwafanya watu kuwa na wivu na kufilisika wakijaribu kuboresha nyumba zao, kabati la nguo, na likizo zifanane na picha hizo. Twitter (ikiwa imefanywa vizuri) huondoa mawazo ya uchu wa mali hadi kwenye maswali makubwa ya kiraia, kifalsafa, na hata ya kiroho. Twitter ni bora zaidi,” Megan Basham alitoa maoni.

Wengine walisema kuwa huenda Musk ameanzisha vita vya ugomvi baina yake na mmiliki wa Instagram Mark Zuckerburg.