Nyeri: Gari dogo lanaswa likisafirisha ng'ombe na ndama walioibwa

Wengi walishangaa ni vipi ng'ombe huyo mkubwa na ndama wake waliweza kutoshea ndani ya gari hilo.

Muhtasari

• “Hii ni ile mbogi ya ‘Ni God Maze’ kumbe watu ni weiz ajabu,” mwingine alisema.

Gari lililonaswa na ng'ombe
Gari lililonaswa na ng'ombe
Image: Facebook

Wikendi iliyopita kioja kilishuhudiwa katika Kaunti ya Nyeri eneo bunge la Kieni baada ya gari dogo aina ya Sienta kupatikana likisafirisha ngombe na ndama wake ambao walikisiwa kuwa wa wizi.

Maafisa wa polisi ambao walishuku jinsi gari hilo dogo lilikuwa likijikokota kwa mwendo wa kinyonga huku nyuma likiwa linajiburura walilisimamisha na kuangalia ndani wakagundua kuwa ni ngombe mkubwa pamoja na ndama wake walikuwa ndani.

Inaarifiwa kuwa gari hilo lilikuwa linatoka eneo la Nanyuki likielekea Nyeri.

Picha hizo zilisambazwa mitandaoni huku mzaha ukizuka kutokana na maandishi yaliyokuwa kwenye gari hilo, “Siri ni maombi”

Watu mitandaoni walishindwa kujizuia kuhusu ujumbe huo kwenye maandishi katika gari la wizi.

“Halafu wanasema eti siri ni maombi ndio tudhani wamebeba kasisi wa kanisa, walaamiwe kabisa,” Gerald Korir alisema.

“Hii ni ile mbogi ya ‘Ni God Maze’ kumbe watu ni weiz ajabu,” mwingine alisema.

“Hakuna Siri nyingini,Siri ni yesu tu watu waache wizi....jaribu kufikiria tu Sienta kubeba ng'ombe mzima na ndama wake,” Abel Serem alishangaa.

Suala la wizi wa mifugo limekuwa donda sugu kwa muda mrefu humu nchini haswa kaika jamii za wafugaji ambapo rais Ruto na waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki wametoa tahadhari kwa wezi hao kujisalimisha kabla serikali haijachukua hatua kali dhidi yao.