UNESCO: 2022 Mwanahabari mmoja alikuwa anauawa kila baada ya siku 4

Shirika hilo lilisema mauaji haya yaliongezeka kwa 50% na kufikisha idadi ya waandishi wa habari waliouawa kazini hadi 86.

Muhtasari

• UNESCO walisema wanahabari wengi waliouawa walitoweka kwa njia za utata na wengine kutekwa nyara na unyanyaswaji wa kisheria.

• Walitoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua mwafaka ili kuwalinda waandishi wa habari kote duniani.

Wanahabari kazini
Wanahabari kazini
Image: MAKTABA

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO limetoa takwimu za ukakasi mkubwa kuhusu ongezeko la vifo vya wanahabari kote duniani katika mwaka uliopita wa 2022.

Kulingana na shirika hilo, vifo vya wanahabari na wafanyakazi wanaohusiana na vyombo vya habari viliongezeka kwa asilimia 50 katika mwaka wa 2022 pekee.

Katika taarifa zilizochapishwa na shirika moja la kimataifa l habari, ongezeko hilo lilimaanisha kwamba kila baada ya siku nne, mwanahabari mmoja alikuwa anapoteza maisha yake katika kuuawa.

"Baada ya miaka kadhaa ya kupungua mfululizo, kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya waandishi wa habari waliouawa mwaka 2022 kunatisha," Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Audrey Azoulay alinukuliwa na  AFP.

Takwimu za mauaji ya waandishi wa habari kati ya mwaka 2019 na 2021 zilikuwa ni vifo 58 lakini katika mwaka 2022, idadi hiyo iliongezeka hadi kufika vifo 86 vya wanahabari.

Shirika hilo lilitoa wito kwa serikali na mamlaka husika katika mataifa mbalimbali ambapo wanahabari wanadhulumiwa kuchukua hatua za kisheria kuwalinda wanahabari.

Walisema kuwa katika visa 86 vilivyoripotiwa, hakuna hata kimoja ambacho haki imetendeka.

"Mamlaka lazima waongeze juhudi kukomesha uhalifu huu na kuhakikisha wahalifu wao wanaadhibiwa, kwa sababu kutojali ni sababu kuu katika hali hii ya vurugu," UNESCO ilitoa wito.

“Sababu za mauaji ya waandishi wa habari ni pamoja na "kulipiza kisasi kwa kuripoti uhalifu uliopangwa, migogoro ya silaha au kuongezeka kwa itikadi kali, na kuangazia masuala nyeti kama vile rushwa, uhalifu wa mazingira, matumizi mabaya ya mamlaka na maandamano," UNESCO iliongeza.

Shirika hilo pia lilisema kuwa kando na mauaji ya wanahabari, wengine wanaweza kukabiliwa na "aina nyingi za unyanyasaji" ikiwa ni pamoja na "kupotea kwa nguvu, utekaji nyara na kuwekwa kizuizini kiholela, unyanyasaji wa kisheria na unyanyasaji wa digital, hasa dhidi ya wanawake.

Itakumbukwa miezi michache iliyopita nchini Kenya, watu waliodhaniwa kuwa walinzi wa mama Dorcas Rigathi ambaye ni mke wa naibu rasi Rigathi Gachagua walinaswa kwenye video wakimdhulumu mwanahabari kwa kumpiga katika hafla ambayo Dorcas alikuwa amekwenda kusambaza vyakula vya msaada kufuatia ukame mkali nchini.

Kitendo hicho kilifokewa vikali na kukashfiwa huku shirika linalosimamia wanahabari nchini MCK likitoa tamko kali la kukashfu unyanyasaji huo.