Aliyekuwa waziri George Magoha apata kazi ya uhadhiri chuo kikuu cha Maseno

Magoha ana tajriba kubwa katika taaluma ya udaktari wa upasuaji, somo ambalo atakuwa anafunza katika chuo hicho.

Muhtasari

• Magoha aliteuliwa kama waziri wa elimu kuchukua nafasi ya Matiang’i aliyehamishwa hadi wizara ya usalama wa ndani na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

George Magoha
George Magoha
Image: Maktaba

Aliyekuwa waziri wa elimu msomi George Magoha amepata kazi nyingine nzuri, miezi mitatu tu baada ya kuondoka wizara ya elimu.

Duru zaarifu kuwa Magoha ambaye alifahamika sana kwa misimamo yake mikali kuhusiana na masuala ya elimu, amepata kazi kuwa mhadhiri wa upasuaji katika chuo kikuu cha Maseno.

Magoha ni msomi mwenye tajriba ya miaka mingi katika taaluma ya udaktari wa upasuaji na amepata kazi ya kufunza somo hilo kwa wanafunzi wa Maseno ambao wanasomea udaktari wa sajari.

"Yeye ni rasilimali kwetu kutokana na uzoefu wake mkubwa na taaluma dhabiti. Shule yetu ya Tiba ni mpya na kupata uzoefu na haiba shupavu kama Magoha hakika ni faida kwetu,” Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma, Dkt McOnyango alinukuliwa na Nation.

Kabla ya kuteuliwa katika baraza la mawaziri miaka mitano iliyopita, Prof Magoha alihudumu kama naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) kwa miaka kumi (2005 hadi 2015).

Pia aliwahi kuwa Profesa wa Upasuaji wa Urolojia na Upandikizaji katika kitengo cha Sayansi ya Afya vhuo kikuu cha nairobi. Kazi yake ya matibabu inajumuisha kazi na mafunzo nchini Nigeria, Ghana, Ireland na Uingereza. Pia alisomea Uongozi Mtendaji katika Chuo Kikuu cha Stanford.

Magoha aliteuliwa kuwa waziri wa elimu kuchukua nafasi ya Matiang’i aliyehamishwa hadi wizara ya usalama katika serikali ya iliyowa ya rais mustaafu uhuru Kenyatta.

Magoha atakumbukwa na wengi kwa kuwa mstari wa mbele kusukuma na kuwarai wazazi kukumbatia mtaala mpya wa elimu – CBC ambapo alifanya ziara nyingi tu kote nchini akizundua ujenzi wa madarasa ya CBC.

Baada ya serikali ya Kenyatta kumaliza hatamu yake, aliondoka na baraza lake la mawaziri na rais Ruto akateuwa mawaziri wapya, Ezekiel Machogu akivivaa viatu vya Magoha katika wizara hiyo.