Jubilee: Raila Odinga alimshinda William Ruto kwa zaidi ya kura milioni mbili

Katibu mkuu wa chama hicho Jeremiah Kioni alitoa hati iliyoonyesha kuwa Odinga alipata 57.33% ya kura dhidi ya 41.665 ya kura za Ruto.

Muhtasari

• Kioni alisema kuwa taarifa hizo za kinyemela zilidokezwa kwake na mtoa taarifa kwa kisiri ambaye alikuwa anafanya kazi katika tume ya IEBC.

JEREMIAH KIONI
Image: ENOS TECHE

Chama cha Jubilee sasa kimeibua madai mapya kikisema kuwa aliyekuwa mgombea urais wa Azimio la umoja One Kenya Raila Odinga alishinda uchaguzi wa urais wa mwaka jana kwa kura nyingi.

Aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni ambaye pia ni katibu wa chama cha Jubilee katika mkutanao na wanahabari Jumatano jijini Nairobi, alisema kuwa ana uhakika mkubwa na mtoa taarifa mmoja kutoka kwa tume ya IEBC ambaye alimfichulia kuwa Odinga alishinda kwa zaidi ya kura milioni mbili.

Kulingana na katibu huyo wa Jubilee, Mtoa taarifa huyo ambaye jina lake halikujulikana alimfichulia kuwa alikuwa kigezo muhimu cha usimamizi wa uchaguzi. Afisa huyo anadai Raila Odinga alipata kura 8,170,355 (57.33%) dhidi ya 5,915,973 za Rais William Ruto (41.66%).

"Taarifa ya kina itatolewa na kiongozi wa chama chetu na wengine ambao mmetuona siku zote ndani ya Azimio na naomba mchukue muda pia kupitia ripoti hiyo, tutawajumuisheni," alisema Kioni.

Taarifa hizi zinakinzana pakubwa na matokeo rasmi ambayo yalitangazwa na Chebukati mnamo Agoosti mwaka jana ambapo William Ruto aliibuka mshindi kwa kupata kura  7,176,141 (50.49) akimbwaga odinga aliyeibuka wa pili kwa kura 6942,930 (48.85).

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Chebukati na wenzake watatu kustaafu rasmi baada ya kukamilika kwa kipindi cha miaka 6 kisicho na kipengele cha kurudiwa upya kulingana na katiba.

Katika hafla ya kustaafu kwao, rais Ruto aliibua madai Makai kuwa kulikuwepo na njama ya kujaribu kuhitilafiana na tume ya IEBC kwa kumteka nyara Chebukati na kumuua ili kamishna mbadala achukue jukumu hilo na kumtangaza mpinzani wake kama mshindi, jambo ambalo rais alisema Chebukati alisimama kidete na kulikataa licha ya kupokea vitisho na ahadi za zawadi nono.