Ma'bouncer wa Kenya wataka serikali kuwaruhusiwa kutumia silaha wakiwa kazini

Mwenyekiti wao Brian Omondi Ongore alisema huwa wanafanya kazi katika mazingira hatarishi.

Muhtasari

• Walitolea mfano kuwa mara nyingi mabouncer wengi hukumbana na watu wanaoingia kwenye sehemu za starehe wakiwa na bunduki na pindi wanapolewa huanza vurugu.

Walinzi wataka kupewa idhini ya silaha
Walinzi wataka kupewa idhini ya silaha
Image: Shutterstock,

Muungano wa ma’bouncer nchini Kenya umetoa ombi kwa serikali kuwaruhusu kubeba silaha kama bunduki wakiwa kazini.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao Brian Omondi Ongore, walinzi hao ambao aghalabu wanafanya kazi kalinzi wa watu mashuhuri na wengine kwenye vilabu vya kifahari walisema kuwa ni wakati umefika sasa wapewe ruhusa ya kumiliki silaha wakiwa kazini.

Ongore alisema kuwa tayari wameanzisha mazungumzo na mamlaka inayosimamia utoaji wa silaha hizo kwa rais katika kile walisema kuwa kila siku wao hufanya kazi katika mazingira hatarishi kutoka kwa watu wanaomiliki silaha kwa njia haramu na baadhi kwa njia halali.

“Tunagongana na wezi, majambazi na wengine na hivyo ni jambo la maana kwa wanachama wetu kupewa mafunzo kuhusu umiliki wa bunduki. Pia tunafanya kazi kwa ukaribu na mamlaka ya utoaji silaha ili pia kutusaidia kutuunganisha na polisi ili tupate mafunzo kama haya,” Ongore alisema.

Alitolea mfano kuwa mara nyingi mabouncer wengi hukumbana na watu wanaoingia kwenye sehemu za starehe wakiwa na bunduki na pindi wanapolewa huanza vurugu.

Katika hali kama hiyo, Ongore alisema ni vizuri mabouncer hao wapewe mafunzo maalum ya jinsi wanaweza kulikabili tishio hili la mtu mlevi ambaye anatamba na bunduki yake, jinsi ya kumnyang’anya bunduki ile na pia jinsi ya kuiweka sehemu salama wakisubiri polisi kufika ili kukabili hali nzima.

Muungano huo pia ulizindua kadi ya utambulisha kwa wanachama wao ambayo itakuwa inatumiwa kuwatambua wakati wako kazini iwe ni kulinda klabu, biashara au mtu mashuhuri kama wanasiasa na wanamuziki.

“Hii kadi itakuwa kama utambulisho mkuu wa wewe kufanya kazi kama bouncer na tunaomba serikali pia itusaidie kuondoa wakora na wezi ambao wanajifanya mabouncer katika hizi sehemu ambazo watu wetu wanafanya kazi,” Ongore alisema akionesha kadi hiyo.