Askofu aliyefariki aibuka akimsajilisha bintiye katika shule ya kutoa msaada kwa mayatima

Miaka 4 iliyopita, askofu huyo mwanamume alimpeleka binti wa kwanza shuleni humo na kumsajilisha kama yatima asiye na baba.

Muhtasari

• Alimwandikisha mtoto wa kwanza akisema hana baba wakati yeye ndiye baba mzazi, kwa njama ya kupata msaada wa bure.

•Safari hii aliporudi, alinaswa na kulazimika kutoroka kwa aibu.

Askofu aliyenaswa akidanganya kuwa ni marehemu
Askofu aliyenaswa akidanganya kuwa ni marehemu
Image: Screengrab

Hali ya mshikemshike ilijiri katika shule moja katika kaunti ya Machakos baada ya mzazi mmoja wa kiume anayetajwa kuwa askofu wa kanisa kumpeleka mtoto wake shuleni ili kumsajili kama yatima asiye na baba.

Kulingana na taarifa iliyopeperushwa kwenye runinga ya Citizen, mchungaji huyo ambaye hakutambulika kwa jina aliongozana na mkewe wakimpeleka mtoto wao katika shule hiyo ya kutoa msaada wa masomo kwa watoto kutoka familia zisizojiweza na mayatima pia.

Iliarifiwa kuwa wazazi hao miaka minne iliyopita walimsajilisha mtoto wao wa kwanza katika shule hiyo wakidai kuwa ni yatima asiye na wazazi.

Na kama ilivyo kawaida ya muonja asali ambaye haonji mara moja, baada ya njama yao kufanikiwa miaka minne iliyopita, tena walirudi kwa mara nyingine wakiwa na mtoto wao wa pili ambaye pia walinuia kumuandikisha kama yatima ili kupokea msaada wa masomo ya bure.

Lakini safari hii, njama yao iligonga mwamba. Citizen waliripoti kuwa wawili hao waligundulika na ikawalazima kukimbilia usalama wao huku wakificha uso wao wa aibu kwa kuanikwa kwa njama yao.

“Wawili hao wanadaiwa kumsajili mwanao wa kike katika shule hiyo ya kuwasaidia wanafunzi kutoka familia maskini miaka minne iliyopita kwa kisingizio kuwa hawajiwezi kwani baba yake mtoto ambaye ni askofu huyo alikuwa amefariki dunia. Waligunduliwa walipokuwa wakimsajili mtoto mwingine tena,” sehemu ya taarifa katika runinga ya Citizen ilisoma.

Baada ya njama yao kutibuliwa, mkurugenzi mkuu wa shule hiyo kwa jina Caring Hearts Group of Schools alisema kuwa sasa askofu huyo anahitajika kisheria kulipa gharama zote za masomo za miaka minne ambazo bintiye wa kwanza amekuwa akipata kama yatima asiye na baba.

"Sasa anatakiwa na washauri wetu wa kisheria kulipa KSh 450,00 ambazo hazitoshi hata kidogo kwa sababu msichana huyu amekuwa hapa na amechukuliwa kwenye safari za masomo na michezo na manufaa mengine mengi ya kuwa Caring Hearts," alisema. alimfadhaisha Vincent Kituku, mkurugenzi wa shule hiyo.