Wakenya 4 akiwemo Uhuru Kenyatta wana utajiri wa bilioni 333 kuliko Wakenya maskini 22M

Wakenya matajiri 130 nchini wana utajiri sawa na 70% ya bajeti ya sasa ya Kenya ambayo ni trilioni 3.3

Muhtasari

• Uchambuzi unaonyesha kuwa kuna watu 1,890 nchini Kenya wenye thamani ya dola milioni 5 (Sh 615 milioni) au zaidi.

• Ripoti hiyo ilisema wale waliokuwa juu mwaka jana kwa utajiri bado ndio wameshikilia nafasi hizo mwaka huu.

Familia ya kina Uhuru Kenyatta yaongoza katika utajiri Kenya
Familia ya kina Uhuru Kenyatta yaongoza katika utajiri Kenya
Image: Maktaba

Kampuni ya kufanya utafiti ya Oxfam imebaini mapya kuhusu utajiri wa Wakenya.

Kulingana na utafiti wao wa hivi karibuni, familia nne tu humu nchini zina utajiri mkubwa zaidi kuliko Wakenya milioni 22.

Oxfam inasema matajiri hao wanne - ambao hawajatajwa - wana utajiri wa Shilingi bilioni 333, ambao ni zaidi ya kile Wakenya milioni 22 maskini zaidi (asilimia 40 ya chini) wanamiliki.

Japo haikutaja majina ya wakwasi hao, itakumbukwa Januari mwaka jana waliwataja wakenya wane ambao walikuwa wanaongoza katika utajiri, familia ya kina rais mstaafu Uhuru Kenyatta ikiwa moja yao.

Jarida la Nation linaripoti kuwa kipindi hicho, Ripoti ya Oxfam mwaka jana iliorodhesha Samir Naushad Merali, Bhimji Depar Shah, Jaswinder Singh Bedi na familia ya Rais wa zamani Uhuru Kenyatta kuwa wanne bora zaidi nchini, wakiwa na utajiri wa Sh311.7 kwa jumla.

Katika ripoti ya mwaka huu Oxfam ilifichua kuwa watu 130 matajiri zaidi nchini Kenya wanamiliki mali sawa na asilimia 70 ya bajeti ya sasa ya nchi ambayo inasimama kwa shilingi trilioni 3.3, au asilimia 19 ya Pato la Taifa (GDP).

“Uchambuzi unaonyesha kuwa kuna watu 1,890 nchini Kenya wenye thamani ya dola milioni 5 (Sh 615 milioni) au zaidi, huku utajiri ukifikia dola bilioni 39.9 (Sh4.9 trilioni). Hii pia inajumuisha watu 130 walio na $50 milioni (Sh6.15 bilioni) au zaidi na utajiri wa jumla wa $18.7 bilioni (Sh2.3 bilioni)," Oxfam ilisema.

Msimamizi wa Mikakati ya Haki ya Fedha katika Oxfam Kenya Andrew Gogo alinukuliwa na jarida hilo akisema kuwa orodha ya watu wane wenye utajiri mkubwa zaidi nchini haijabadilika kutoka ile ya mwaka jana, ila akasema utajiri wao huenda umeongezeka kwa kiasi kuliko ule wa mwaka mmoja uliopita.