Mwanamke Mkenya aanzisha tovuti ya kuchumbiana, malipo ya kujiunga ni elfu 5 kwa miezi 3

Alisema kuwa ana imani ya juu kwamba ndani ya miezi 3 ya uanachama, mtu utakuwa umeshapata mwenza wako.

Muhtasari

• Hata hivyo, wengi waliiba maoni kinzani mitandaoni wakimuita mlaghai na wengine wakimtupia matusi.

• Amakove aliweka msimamo wake wazi kuwa hababaishwi na matusi ya watu na kuwa lengo lake litaendelea kawaida.

Mwanaharakati Amakove Wala aibua maoni kinzani akizindua tovuti ya kuchumbiana
Mwanaharakati Amakove Wala aibua maoni kinzani akizindua tovuti ya kuchumbiana
Image: Facebook

Mwanaharakati Dkt Amakove Wala amegonga vichwa vya habari wikendi iliyopita baada ya kutangaza kufungua tovuti ya watu kupata wenza wao katika mtandao wa Telegram.

Kuanzisha kundi kama hilo kwenye mtandao wa Telegram hata hivyo si shida, gumzo kubwa lilikuwa pale aliposema kuwa ili kuwa mwanachama, hautajiunga bure bali ni sharti mtu uzame mfukoni mwako na kutengana na kiasi cha shilingi elfu 5 pesa za Keya ili kuwa mwanachama kwa miezi 3 tu!

“Hey watu wazuri. Hatimaye tayari kwa Klabu ya Mitandao ya SYS kwenye Telegramu pekee. Usajili ni 5000/- kwa miezi 3. Tunaamini kuwa ndani ya miezi hiyo 3 unapaswa kuwa unapiga gumzo na mtu. Hii sio dhamana,” Amakove aliandika.

Aliendelea mbele na kutoa masharti makali yatakayomfanikisha mtu kuwa mwanachama wa kikundi hicho na kutoa till kwa ajili ya malipo kujiunga.

“Sheria ni: unatoa umri, jinsia, eneo na hali ya ndoa. Ikiwa habari unayotoa itathibitishwa kuwa kinyume, utafukuzwa bila marejeleo zaidi. Mengine ni juu yako kushiriki katika kikundi au na mtandao. Mara tu unapolipa, shiriki mawasiliano nami kupitia Telegramu iongezwe kwenye Klabu ya Mitandao ya SYS. Wasifu mmoja tu kwa kila mwanachama utaongezwa. Maelezo zaidi yatashirikiwa baadaye,” alifafanua.

Baada ya tangazo hili, watu walimsuta kwenye mitandao ya kijamii, baadhi wakimuunga mkono kwa hatua hiyo.

Wengine walienda mbele na kumtukana kwa maneno ya nguoni, jambo ambalo halikuonekana kumbabaisha hata kidogo huku akijieleza kuwa baadhi ya matusi hayo kwake ni kawaida sana na wala hayampi kiwewe.

“Nimeachika. Kwa ufafanuzi wa kisheria. Mimi ni mtu wa nje na ninazungumza mawazo yangu. Mimi ni mwanamke. Ninapenda ngono. Ninapenda wanyama. Nawapenda watoto wangu. Ninapenda kusafiri. Nina tamaa. Ninaendesha biashara kadhaa. Mimi ni daktari. Mimi ni mwanaharakati. N.k. Hivi vyote ni vivumishi vya kunielezea. Unaona, lebo hutumiwa na watu ambao wana hofu ya ndani wenyewe. Tunaweka majina ya watu ambayo sisi wenyewe tunapambana nayo. Kwa hiyo ukisema Amakove ameachika. Unasema ukweli,” aliandika katika moja ya chapisho lake.