Pastor Dorcas Gachagua awatupia lawama walimu kwa kulea watoto wa LGBTQ shuleni

"Nyinyi walimu hamtaki kulizungumzia suala la LGBTQ shuleni kwa sababu mnataka kuonekana wazuri, huku watoto wenu wakienda motoni"

Muhtasari

• Nyinyi muonekane vizuri lakini mkiacha watoto wenu waende kuzimuni - Dorcas Gachagua.

Mama Dorcas Gachagua
Mama Dorcas Gachagua
Image: Facebook

Mama Dorcas Gachagua ambaye ni mchungaji ametupa neno la lawama kwa wazazi na walimu shuleni kwa kuficha visa vya ushoga na usagani katika sehemu hizo ambazo siku za nyuma zilikuwa zinaonekana kama sehemu salama za kuwafunza watoto maadili mema katika jamii.

Akizungumza wikendi iliyopita, mchungaji Dorcas alisema kuwa walimu wanafaa kuwa katika mstari wa mbele wakishirikiana na wazazi ili kukomesha hulka za watoto kujiunga na jamii ya LGBTQ na vyama vinavyofagilia mapenzi ya jinsia moja.

“Nyinyi walimu mnajua kuwa hivi karibuni tumekuwa na visa vya watoto wetu kujihusisha na usagaji na ushoga. Na hili ni jambo ambalo hamtaki kulizungumzia hadharani kwa sababu mnataka kuonekana wazuri. Nyinyi muonekane vizuri lakini mkiacha watoto wenu waende kuzimuni. Hiki ni kitu ambacho sharti tukibadilishe kama walimu,” Dorcas Gachagua alisema.

Alisema kuwa atahakikisha anatumia ushawishi wa ofisi yake kama mke wa naibu rais kuhakikisha uchamungu umedumishwa katika shule, taasisi na idara mbali mbali za kiserikali katika ngazi zote ili kuhakikisha watoto hawapotelei kwa masuala ya LGBTQ ambayo aliyataja kama ya kidunia.

Alisema pia kuwa mahubiri ya uchamungu yataenezwa si tu katika taasisi za kimasomo bali pia katika idara mbali mbali za kiserikali ambazo zinajumuisha vijana ili kuwaokoa kutoka kwa kupotelea mambo ya kidunia.

“Taasisi kama za Kipolisi na magereza yana uhaba katika masuala ya uchamungu na ushauri nasaba na ndio maana viana wengi haswa vijana wa kiume ambao nina shauku nao wanapotea kwa kujiua kutokana na unyongovu kwa kukosa muongozo dhabiti. Wanahitaji mafunzo ya kidini ambayo yatawatia moyo na kuwapa Imani,” Mchungaji Dorcas alisema.

Awali, alisema kuwa alitembelea ofisi ya inspekta jenerali wa polisi Japhet Koome ambayo walizungumzia mengi kuhusu kuwakimu vijana wanaohudumu katika idara za polisi, likiwemo suala la kusimamia harusi za wale ambao wangetaka kuoa.

Tamko lake kuhusu LGBTQ shuleni linakuja wakati ambapo taasisi za kimasomo nchini zimetuhumiwa kwa kuruhusu watoto kujifunza mambo kama hayo shuleni. hili ni kufuatia kifo cha aliyekuwa mwanaharakati wa LGBTQ Edwin Chiloba wa chuo kikuu cha Eldoret, jambo ambalo pia limeshrutisha chuo hicho kuweka sheria kali kuhusu mavazi ya wanafunzi wake.