Ruto awakaribisha Sabina Chege na Kanini Kega wa Jubilee katika ikulu ya Nairobi

Chege na Kega walikuwa wakosoaji wakuu wa sera za Ruto katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Muhtasari

• Chege hakuwania wadhifa wowote katika uchaguzi wa mwaka jana huku Kega akiwania kiti cha ubunge wa Kieni lakini akapoteza.

• Kwa sasa, Kega ni mbunge wa EALA.

Kenya Kwanza yawakaribisha Wabunge wa Jubilee
Kenya Kwanza yawakaribisha Wabunge wa Jubilee
Image: Twitter

Mtandao wa Twitter Jumatatu asubuhi uliseheneni gumzo pevu linalomhusu mbunge wa kuteuliwa Sabina Chege baada ya kupakia picha ya pamoja akiwa na rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua katika ikulu ya Nairobi.

Katika picha hiyo ambayo alipakia bila kuandika kitu chochote, Chege alionekana amesimama katikati ya vigogo hao wa Kenya Kwanza huku uvumi ukiibuka kuwa amebwaga manyanga katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na kuingia mrengo wa Kenya Kwanza.

Itakumbukwa kuwa Sabina Chege alikuwa ni mwakilishi wa kike wa Murang’a kupitia tikiti ya chama cha Jubilee na katika uchaguzi wa mwaka 2022, aliamua kujiunga na Azimio.

Baada ya kujiunga na kambi ambayo kiongozi wa chama chake Uhuru Kenyatta alikuwa anapigia debe, Chege aliamua kutowania wadhifa wowote katika uchaguzi huo huku za ndani zikidai kuwa alikuwa ameahidiwa nafasi nzuri katika serikali endapo Azimio wangeibuka washindi kupitia kinara wao Raila Odinga.

Chege alikuwa katika mstari wa mbele kunadi sera za Odinga haswa katika eneo pana la Mlima Kenya lakini miezi mitatu na ushee sasa tangu kukamilika kwa uchaguzi na Odinga kupoteza, Chege amekuwa mchache sana kuonekana akizungumza hadharani kuhusu siasa za Azimio.

Chege aliongoza wanasiasa wengine kutoka eneo la Mlima Kenya ambao walikuwa wakiunga mkono Azimio, kwenda ikulini ambapo walionekana katika picha ya pamoja, akiwemo mbunge wa EALA Kanini Kega ambaye alikuwa mbunge wa Kieni.

Wengine ni pamoja na mbunge wa Embakasi West Mark Mwenje, mbunge wa Starehe Amos Mwago, Daniel Karito wa Igembe, Stanley Muthama, Joseph Githuku wa Lami miongoni mwa wengine ambao walikuwa Azimio.