Bungoma: Mazishi yasitishwa wanawake 3 wakipigania mwili wa mume wao

Mzee mmoja alisema jeneza hilo sasa halitatumiwa kumzika mzee kwani ni kinyume cha tamaduni jeneza kurudi bila mwili.

Muhtasari

• Walizozania mwili wa marehemu katika chumba cha mochwari jambo lilipelekea kunyimwa mwili na kurudi nyumbani na jeneza tupu.

Mazishi Bungoma yasitishwa wake wakigombania mwili wa mume
Mazishi Bungoma yasitishwa wake wakigombania mwili wa mume
Image: Screengrab//Citizen TV

Shughuli za mazishi katika eneobunge la Webuye kaunti ya Bungoma ziligoma kuendelea baada ya wanawake watatu ambao wote walikuwa wameolewa na mwanamume marehemu, kila mmoja kudai haki ya kuzika mwili wa mume wao.

Kulingana na ripoti iliyopeperushwa katika runinga ya Citizen, wake hao watatu walianzisha zogo la kulaumiana kuhusu matukio yaliyojiri kabla ya mazishi yake, kila mmoja akisema alikuwa wa mwisho kutumia dakika za marehemu za mwisho naye.

Wazee katika kijiji hicho waliwataka wanawake hao wote kusuluhisha tofauti zao kabla ya mzee kuzikwa ili kukwepa mikosi ambayo huenda ikawaandama, kwani ni kinyume cha mila na tamaduni kwa jeneza kurudishwa nyumbani bila mwili, hivyo jeneza hilo haliwezi kutumiwa kumzika mzee.

“Na sisi kwa kimila ya Waluhya au Wabukusu, huwezi leta jeneza kwa boma bila mwili. Sasa hilo jeneza litarudi huko na halitatumika wakati kesi itakapokuwa imeisha,” alisema mzee mmoja.

Inaarifiwa kuwa mke wa tatu alimtuhumu mke wa kwanza kwa na kumtaka kukaa mbali na mazishi kwa kile alisema kuwa hakuwahi mhudumia kipindi anaugua.

Kwa mujibu wa tamaduni za Waluhya kutoka kaunti hiyo ya Bungoma, itabidi mwili wa mzee huyo ukarudishwa katika makafani na jeneza jingine kununuliwa baada ya kuonekana wake hao watatu kila mmoja alitaka kupewa haki ya kumzika mzee.

Mke mmoja ambaye alizungumza na runinga hiyo alisema kuwa yeye hakuwa na shida yoyote kwani alitaka kumpumzisha mzee wake akisema kuwa aling’ang’ana naye hospitalini hadi akafia mikononi mwake.

“Mimi sina shida, wakiamua kuzika mzee, wacha mzee azikwe hatutaki vita, tunataka kuzika mzee wetu kwa amani kwa maana alikuwa mtu wa furaha. Haijalishi alikufa kwa mikono yangu kwa sababu nilishughulika na yeye mpaka dakika ya mwisho.”