Chuo Kikuu ambacho kimekosa wanafunzi kwa miaka 13 licha ya kuwa na kila kitu

Profesa mmoja alihamishiwa katika chuo hicho ili kuwa VC lakini alistaafu baada ya miaka 8 bila kuona mwanafunzi hata mmoja.

Muhtasari

• Chuo hicho kimwekuwa na wahadhira wote kwa miaka hiyo yote lakini hakuna mwanafunzi hata mmoja amewahi jitokeza kujiandikisha kule.

• Katika muda huo wote, chuo hicho kimekuwa kikipokea fedha za maendeleo kutoka kwa serikali bila kutoa huduma yoyote, kwani hakuna wanafunzi.

Mchoro wa chuo kikuu
Mchoro wa chuo kikuu
Image: The Citizen

Mtu akikuhadithia kuhusu chuo au taasisi yoyote ya serikali ambayo ni ya kutoa masomo ya mtaala halali kukosa mwanafunzi hata mmoja kwa zaidi ya miaka 10, utaona kama ni hekaya za Abunuwasi na sufiria zake za kuzaana.

Lakini hili ni tukio ambalo ni la uhalisia kabisa.

Nchini Tanzania, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo wilaya ya  Butiama, eneo la Mara kimekuwa bila mwanafunzi hata mmoja kwa miaka 13 iliyopita licha ya kuwa na wahadhiri wote pamoja pia na kupokea hela za maendeleo ya chuo katika kipindi hicho chote.

Najua bado hili haliingii akili mwa watu wengi lakini ukweli ndio huo ambao ulibainika baada ya kamati ya bunge ya maendeleo ya jamii nchini Tanzania kutembelea na kukagua maendeleo ya chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 2010.

Wajumbe wa kamati hiyo walionekana kushangazwa na wengine kukerwa na hali ya taasisi hiyo ya elimu ya juu.

“Mkuu wa chuo na wafanyakazi wako nawaonea huruma sana, mmeteswa muda mrefu sana kwa kuwekwa Butiama miaka yote bila wanafunzi, haya ni mateso,” alinukuliwa mjumbe Bi Husna Sekiboko wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma.

Kama hayo madhira hayatoshi, inaarifiwa kuwa kuna profesa mmoja aliyepelekwa chuoni humo kuwa Makamu Mkuu wa chuo na alistaafu baada ya miaka minane bila hata kutoa mhadhara mmoja, kwani hakukuwa na mwanafunzi hata mmoja wa kufunza ndani ya miaka yake 8 kama VC.