Mtoto wa kiume wa miezi 6 apatikana ametupwa kwenye shamba la mahindi

Wakaazi walisikia mtoto akilia na walipofika walimkuta ametupwa hapo na kando yake kulikuwa na nguo zake.

Muhtasari

• Chifu wa eneo hilo alisema uchunguzi wa awali ulionesha mtoto huyo huenda alitupwa na msichana wa chuo kikuu.

Image: BBC NEWS

Mtoto wa miezi 6 alipatikana ametupwa katika shamba la mahindi huko Tigania Magharibi kaunti ya Meru siku ya Jumatatu.

Kulingana na taarifa kutoka kwa chifu wa eneo hilo Lucy Kambanja, wanakijiji walisikia sauti za mtoto akilia kutoka shambani kwa mfululizo na walipofika, walipata ni mtoto wa miezi sita ametupwa hapo na kandi yake kulikuwa na nguo.

Mtoto huyo aliokolewa na kuwekwa chini ya ulinzi wa msamaria mwema huku chifu akisema kuwa uchunguzi wa awali ulionesha kuwa huenda ni mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu alimtupa mwanawe katika shamba hilo.

Wazazi walilaani tukio hilo huku wakitoa wito kwa kina mama haswa wasichana kutowatupa watoto wao na badala yake kuwalea au kuwapeleka kwa mamlaka husika za kulea watoto kuliko kutupa mtoto shambani kwani ni kutahadharisha maisha yake kutokana na wanyama kama mbwa.

Uchunguzi dhidi ya mama mwenye mtoto huyo ulianzishwa mara moja ili kumtia hatiani kwa kuhatarisha maisha ya kiumbe asiye na hatia.

Kisa hicho kinatokea siku chache baada ya wakaazi katika kijiji cha Gacuku kaunti ya Embu kumpata mtoto mchanga ameuawa kwa kukatwa kichwa na mwili wake ukiwa umetupwa katika shamba la maharagwe.

Mama mmoja mmiliki wa shamba hilo la maharagwe ndiye alipata mwili huo wakati akiwa shambani mwake akivuna maharagwe.

Mwili wa mtoto huyo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti huku uchunguzi ukianzishwa kubainisha waliofanya kitendo hicho na pia kutafuta kichwa chake.