Nakuru:Mwanamke wa miaka 25 ajifungua watoto 5 kwa mpigo, mumewe aomba msaada

Huu ndio ulikuwa ujauzito wa kwanza kwa Margret Wairimu mwenye miaka 25.

Muhtasari

• Daktari alisema mama huyo na wanawe watano bado wako katika hospitali hiyo katika hali shwari.

Image: Maktaba

Mwanadada mmoja ambaye alikuwa amebeba ujauzito wake wa kwanza kabisa maishani mwake alishangaza watu na madakatari katika hospitali ya Nakuru baada ya kujifungua watoto watoto kwa mkupuo.

Taarifa kutoka kwa daktari wa hospitali hiyo ya kiwango cha 5 zilisema kwamba mama huyo mpya mwenye umri wa miaka 25 alikimbizwa katika chumba cha kina mama kujifungua baada ya kugundua kuwa alikuwa amebeba watoto watano tumboni ambao wote walikuwa wamefika muda wao wa kuzaliwa.

Daktari huyo alisema kuwa mama na watoto wake watano sasa wako katika siha nzuri kwenye hospitali hiyo.

Huku tukio hilo ambalo ni nadra sana kutokea likizidi kugonga mawimbi ya mitandao ya kijamii, mwanamume ambaye sasa ni baba mpya kwa watoto hao watano alifikiwa na kituo kimoja cha runinga humu nchini.

Simon Kinyanjui alisema hata yeye hakuwa anatarajia mkewe angejifungua watoto watano kwa mara moja huku akitoa wito kwa wasamaria wema kumpa msaada wa kuwalea watoto hao mapacha watano.

“Nahitaji msaada kwa sababu sikuwa nategemea kabisa kuwa mke wangu angejifungua mapacha watano.”

Taarifa za mama kujifungua watoto 5 mapacha huwa ni nadra sana kutokea na tukio hilo linapotokea huwa ni hadithi kubwa ajabu.

Miezi mitatu iliyopita tuliripoti kuwa mwanadada mmoja ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu nchini Nigeria alishangaza madaktari baada ya kujifungua watoto watano kwa mpigo.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa na Staelitte huko Nigeria, mwanafunzi huyo kwa jina Oluomachi Linda Nwojo, aliwakaribisha watoto hao mwendo wa saa tatu usiku wa Jumatatu, Oktoba 3, mwaka jana.

Binti huyo wa miaka 24 alipata mapacha 5 wakiwemo wa kiume wawili na mabinti watatu, na ndio mara ya kwanza kutokea katika kituo hicho cha hospitali, kulingana na ripoti hiyo.