Sifuna amsuta Chebukati baada ya kutishia kumshtaki Raila

Chifu wa Azimio pia alidai makamishna hao walimwomba kitu kidogo na kwamba ana ushahidi.

Muhtasari
  • Haya yanajiri baada ya wakili Steve Ogolla kutoa barua ya kumtaka Raila kutoa ushahidi wa ziara ya mwenyekiti huyo wa zamani nyumbani kwake ndani ya siku saba
Mgombea useneta wa Nairobi kwa tiketi ya ODM Edwin Sifuna
Image: TWITTER// EDWIN SIFUNA

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amesema kuwa hakuna kitakacho mzuia wakili Steve Ogolla kumwakilisha mwenyekiti mstaafu wa IEBC Wafula Chebukati dhidi ya Chifu wa Azimio Raila Odinga.

Sifuna kupitia akunti yake ya twitter Jumatano alisema kuwa "ila kwa ada za kisheria, hakuna kitu kingine kitakachotoka kwenye tukio hilo la kisheria".

"Yote anayofanya Steve Ogolla ni yale ambayo mawakili hufanya vyema zaidi. Kumsaidia Chebukati kutumia pesa nyingi za kustaafu alizopokea kutoka kwa walipa ushuru," Seneta huyo alisema.

Haya yanajiri baada ya wakili Steve Ogolla kutoa barua ya kumtaka Raila kutoa ushahidi wa ziara ya mwenyekiti huyo wa zamani nyumbani kwake ndani ya siku saba.

Ogolla alitishia kumshtaki Raila, kwa niaba ya Chebukati, kuhusu kauli yake wakati wa mkutano wa Jumapili wa Jacaranda ambapo alidai kuwa Chebukati na makamishna wa zamani Abdi Guliye na Boya Molu walimtembelea nyumbani kwake kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Chifu wa Azimio pia alidai makamishna hao walimwomba kitu kidogo na kwamba ana ushahidi.

Chebukati hata hivyo alikanusha madai ya Raila.