Urafiki wa chuoni: Mwanadada ashirikiana na mpenziwe kumteka nyara rafiki yake

Faith Mwende, rafiki wa karibu wa Daisy Chebet alishirikiana na mpenzi wake Simon Akuteka na kumteka nyara Chebet.

Muhtasari

• Baada ya kumtekqa nyara, Mwende na mpenzi wake waliungana na wanaume wengine wawili kabla ya kutoroka naye kutoka Nakuru kwenda Kiambu.

• Walipigia familia yake simu wakitaka laki 6 ili kunusuru maisha ya mwanao Chebet.

Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Egerton ambaye alitekwa nyara siku tano zilizopita hatimaye alinusuriwa kutoka mikononi mwa watekaji nyara wake siku ya Jumanne Januari 31 na makachero wa DCI katika kaunti ya Kiambu.

Daisy Chebet Barno, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika chuo hicho chenye makao yake jijini Nakuru alidaiwa kutekwa nyara na wanaume watatuwakishirikiana na mrembo mmoja katika eneo la Kabarak kaunti hiyo ya Nakuru na walidaiwa kusafiri naye kuelekea jijini Nairobi.

Simon Akuteka, 39, John Mbau, 38, Elijah Chege, 31 na Faith Mwende walikamatwa katika ghorofa ya Airbnb huko Ruiru.

Mshukiwa huyo wa kike kwa jina Faith Mwende ni rafiki wa akribu wa mwathiriwa Daisy Chebet na ndiye alifanya ushirikiana na wanaume hao watatu, mmoja akiwa mpenzi wake, baadae njama yao iliiva na kumteka nyara rafiki yake.

Siku ambayo alitekwa nyara, Bi Chebet alialikwa kwa chakula cha mchana Kabarak na mpenziwe Bi Mwende aliyetambulika kama Bw Simon Akuteka.

Mara wawili hao wakiwa ndani ya gari Bw Akuteka aliendesha gari kuelekea Kabarak kuchukua kifurushi. Hata hivyo, njiani, waliungana na wanaume wengine wawili. Watatu hao walimfahamisha Bi Chebet kwamba walikuwa wamemteka nyara na kudai fidia ya Shilingi laki 6 kutoka kwa familia yake.

“Watatu hao walisafiri kwa gari hadi Ruiru hadi OJ Restaurant ambako walipanga Airbnb ya vyumba viwili na kumfungia Bi Chebet katika mojawapo ya vyumba vya kulala. Mwende ambaye alikuwa amejiunga nao alichukua chumba kingine cha kulala ambako walifurahia na mpenziwe baada ya Bi Chebet kutuma Sh50,000,” taarifa ya DCI ilisoma kwa sehemu.

Hata hivyo, maafisa wa upelelezi ambao walikuwa wamepokea simu ya huzuni kutoka kwa familia ya Bi Chebet waliwatafuta wanne hao wanaoendesha shughuli zao kati ya Thika, Murang’a, Kajiado na Ruiru mchana.

Wapelelezi walio katika Ofisi ya Utafiti wa Uhalifu na Ujasusi waliwavamia wanne hao katika nyumba iliyokodishwa. Washukiwa hao walikaidi amri ya kujisalimisha na kuwakabili maafisa hao katika mapigano ya ngumi.