Machakos: Kisa cha mwanamke aliyeuza shamba lake kwa mamilioni ya pesa akiwa kaburini

“Justina Mueni alifariki Agosti 7, 2005, lakini, kwa mujibu wa rekodi za Wizara ya Ardhi, Julai 28, 2007, aliuza ardhi yake."

Muhtasari

• Mwanamke huyo alikuwa amemuachia mkwe wake shamba hilo ambalo baadae lilikuja kunyakuliwa na miradi kufanywa pasi na kujulishwa kwa mkwe mwenye shamba.

Kaburi
Kaburi
Image: Maktaba

Shamba moja katika eneo la Syokimau viungaji mwa mji wa Nairobi liko katikati ya mzozo mkali wa kesi baada ya kudaiwa kwamba mmiliki wake ambaye ni mwanamke aliyefariki, alifufuka na kulipiga mnada shamba hilo kabla ya kufa tena.

Jarida moja la humu nchini liliripoti kuwa iliarifiwa mwanamke huyo marehemu alifufuka miaka miwili baada ya kufa kisha akaligawanya shamba hilo kabla ya kubadilisha umiliki wake kwenda kwa watu ambao wanadai walilinunua.

“Justina Mueni alifariki Agosti 7, 2005, lakini, kwa mujibu wa rekodi za Wizara ya Ardhi, Julai 28, 2007, aliuza ardhi yake kwa Exotic Home Properties Ltd, ambayo ina maana wakati wa kusaini uhamisho wa umiliki, alikuwa ameaga dunia,” jarida hilo liliripoti.

Hiki ndicho kipande cha ardhi ambacho alikuwa amemwachia mkwewe, Bw Constantino Mutua. Anasema, Februari 6, 1992, aliingia mkataba wa kuuza ardhi kati yake na mama mkwe wake. Kila kitu kilikuwa sawa hadi ghafla Bi Mueni aliugua na kufa.

Alimwendea baba mkwe wake Joseph Kalani Mutuku, ambaye pia amefariki, na kumwomba apate barua zinazofaa za usimamizi na aanzishe uhamisho wa ardhi hiyo kwake.

Hata hivyo, baba mkwe alionekana kusita kupata barua za uongozi ili kumwezesha kukamilisha shughuli aliyoanza na mkewe marehemu.

Mnamo 2005, Mutua alihamishwa kutoka Nairobi hadi Kisumu kikazi wakati huo, aliacha nyumba moja ambayo ilikuwa haijakamilika kwenye shamba lake.

Mnamo 2009, alitembelea shamba lake na mipango ya kumaliza ujenzi wa nyumba yake na kuanza miradi mingine. Kwa mshangao wake, mgeni alikuwa tayari amenunua na kumaliza kujenga nyumba yake na pia kulikuwa na miundo mingine kadhaa iliyosimama ndani ya kiwanja chake, jarida hilo lilisimulia.