Mashabiki wakabiliwa na mashtaka ya mauaji baada ya wafuasi wa Arsenal na Man city kupigana

Polisi walisema katika taarifa kwamba washukiwa wawili walikuwa kizuizini.

Muhtasari

•Mwanamume mmoja aliuawa katika mji mkuu wa Uganda, Kampala kufuatia mzozo wa matokeo ya mechi nchini Uingereza.

•Polisi walisema katika taarifa kwamba washukiwa wawili walikuwa kizuizini.

Hivi majuzi mashabiki wa Arsenal walikamatwa nchini Uganda kwa kusherehekea barabarani bila kibali
Hivi majuzi mashabiki wa Arsenal walikamatwa nchini Uganda kwa kusherehekea barabarani bila kibali
Image: BBC

Mashabiki wawili wa soka nchini Uganda wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji baada ya mwanamume mmoja kuuawa katika mji mkuu, Kampala kufuatia mzozo wa matokeo ya mechi nchini Uingereza.

Mshauri huyo wa vijana alifariki kutokana na majeraha ya kuchomwa kisu baada ya kuingilia kati kuamua zogo la mashabiki baada ya Arsenal kushindwa na Manchester City siku ya Ijumaa.

Allan Kakumba alifariki muda mfupi baada ya kulazwa hospitalini siku iliyofuata, gazeti la Daily Monitor linaripoti.

Polisi walisema katika taarifa kwamba washukiwa wawili walikuwa kizuizini.

"Tutamfikisha mshukiwa mahakamani hivi karibuni," Luke Oweyesigire, msemaji wa Polisi wa jiji la Kampala, aliambia BBC.

Bw Oweyesigire alisema Bw Kakumba, 25, aliingilia kati wakati kakake Titus Kyendo, shabiki wa Arsenal, aliponaswa katika vita na wafuasi wa Manchester City.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya shabiki wa Arsenal kupigwa hadi kufa huko Adjumani katika wilaya ya West Nile.

Richard Ukuyo alipigwa rungu kisogoni baada ya kumkasirisha mfuasi wa Manchester United aliyeghadhabishwa na ushindi wa Arsenal dhidi yao mwezi uliopita.