Mbona bunge la kitaifa haliko kwenye mtandao wa TikTok? - MP John Kiarie ahoji

Kiiarie alisema wakati umefika bunge hilo kuchukua fursa ya mitandao ya kijamii ambapo Wakenya wengi wamehamia.

Muhtasari

•Ujio wa utandawazi umefanya watu wengi kuhamia mitandao ya kijamii kwa habari na burudani, huku wachache wakibaki kufuatilia shughuli za bunge kwenye redio, TV na magazeti.

Mbunge Kiarie ataka bunge kuwepo Tiktok
Mbunge Kiarie ataka bunge kuwepo Tiktok
Image: Facebook

Mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie amepigia upato ujio wa mitandao mipya ya kijamii huku akihoji ni kwa nini bunge halina ukurasa wao kwenye mtandao mpya wa Tiktok.

Mbunge huyo ambaye ana weledi mpana katika masuala ubunifu alisema kuwa ni wakati sasa wabunge wote wakumbatie utandawazi ambao umerahisishwa na ujio wa majukwaa ya kidijitali ili kujieleza vizuri zaidi.

Mbunge huyo alisema kuwa kitu pekee ambacho kinahitajika ni kupata uelewa wa wale ambao wanalengwa na maudhui ya bunge na hivyo itakuwa rahisi kwa kupakia video zenye kukidhi mahitaji ya walengwa.

“Tunajua jinsi ya kujenga maudhui, kila mbunge hapa ni mkuza maudhui katika kila kitu unafanya, maisha yake, kazi zako kwenye eneobunge, maudhui yamejaa. Majukwaa na mitandao ni mingi zaidi. Tunafaa kukata vipande vifupi vifupi na kupakia kwenye chaneli za Bunge mitandaoni kote. Mbona Bunge hatuko kwenye Tiktok? Tuna kila sababu ya kuwa kwenye Tiktok,” alisema

Mbunge huyo alikashifu jinsi ambavyo kurasa za mitandao ya kijamii ya Bunge la kitaifa inaendeshwa, akisema kuwa ni njia ambayo haiwezi kuwavutia Wakenya kuifuatilia kwa maudhui yake.

Kwa mfano alizungumzia video ndefu za saa nane ambazo zilipakiwa jana na kusema kuwa hakuna mtu ataketi kufuatilia video ndefu kiasi hicho, huku akishauri kuwa video hizo zinafaa kuhaririwa nqa sehemu zenye maudhui mazuri kupakiwa mitandaoni kote kwa ufupi.

Pia alimpongeza mbunge wa Mumias East Peter Salasya kwa kuendesha kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa weledi mkubwa na maudhui ambayo yanawaunganisha wafuasi wake.

“Kila mtu anafaa kuangalia kurasa za mitandao ya kijamii ya Peter Salasya na muone kile ambacho anakifanya, ameunda maudhui mengi ambayo yanawafurahisha watu na hilo limemjengea ufuasi mkubwa kwa miezi michache sana,” Kiarie alisema.