Ruto akutana na viongozi wa Luo Nyanza ikulu, Odinga akiendelea kutomtambua

Rais Ruto akutana na viongozi wa Luo Nyanza kwenye ikulu huku Odinga akiendeleza kampeni za kutotambua uongozi wake.

Muhtasari

• Ni lazima tujitahidi kuongoza kwa mfano na kutumikia maslahi ya watu - Ruto alisema.

Viongozi wa Luo Nyanza wakiwa ikuluni Nairobi.
Viongozi wa Luo Nyanza wakiwa ikuluni Nairobi.
Image: Twitter

Jumatatu rais William Ruto alikutana na viongozi waliochaguliwa kutoka eneo pana la Luo Nyanza katika ikulu ya Nairobi, siku moja tu baada ya kigogo wa kutoka eneo hilo Raia Odinga akiendeleza kampeni zake za kutotambua uongozi wa Ruto katika eneo la Kibera kaunti ya Nairobi.

Katika picha ambazo rais Ruto alipakia kwenye ukurasa wake wa Twitter, viongozi hao Zaidi ya watano wote ni wale ambao wamechaguliwa kama wabunge, wengi wakiwa ni kutoka chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.

Wanasiasa Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki, Independent) Felix Odiwuor almaarufu Jalang'o (Lang'ata), Paul Abuor (Rongo) , John Owino (Awendo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda walihudhuria mkutano huo na rais.

Ruto alisema kuwa kukutana na viongozi hao ni njia moja ya kujaribu kuhakikisha kwamba maendeleo yanapewa kipaumbele na si mambo ya siasa ambazo zilikamilika mwaka jana.

“Viongozi lazima washikane mikono, waendeleze kuishi pamoja na kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi yetu. Ni lazima tujitahidi kuongoza kwa mfano na kutumikia maslahi ya watu. Hii ni njia ya uhakika kuelekea Kenya iliyoungana na iliyoendelea,” rais Ruto alisema.

Rais alisema kuwa mkutano wake ulikuwa unaangaziwa hatua ambazo zimepigwa kimaendeleo katika eneo la Nyanza, wiki chache baada ya kufanya ziara rasmi ya maendeleo katika eneo hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likijulikana kama ngome ya upinzani.