Shabiki wa Man U afariki ghafla baada ya kichapo cha mabao 7-0 dhidi ya Liverpool

Ripoti ilisema kwamba Eddy Okello alilala usiku wa Jumapili baada ya mechi na siku iliyofuata, alipatikana amefariki kitandani mwake.

Muhtasari

•Baada ya kurudi nyumbani kutoka kutazama mechi, Mama yake alimpakulia chakula lakini hakuweza kula.

• Alisema hakuwa anahisi vizuri na kuondoka kwenda kulala, lakini kesho yake alipatikana amefariki.

Polisi
Image: Maktaba

Kufuatia kichapo cha dharau ambacho Machester United walipokezwa mikononi mwa Liverpool wikendi iliyopita, madhara ya kichapo hicho kwa mashabiki yanaendelea kushuhudiwa na kuripotiwa sit u barani Ulaya bali kote duniani.

Nchini Uganda, polisi wameanzisha uchunguzi kufuatia kifo cha kutatanisha cha shabiki wa Manchester United aliyekufa ghafla baada ya kutazama wakibebeshwa kibano cha mabao 7 mikononi mwa Liverpool.

Kulingana na Monitor la Uganda, kisa hicho kiliripotiwa ukanda wa Kaskazini jiji la Lira.

“Eddy Okello, dereva na mkazi wa Okwor Okwor Cell, Wadi ya Burlobo katika Tarafa ya Jiji la Lira Mashariki, alipatikana amefariki chumbani kwake Jumatatu alasiri,” Jarida hilo liliripoti.

Uchunguzi wa awali wa polisi ulionyesha kuwa Okello aliondoka nyumbani mwendo wa saa sita Machi 5, 2023 kwenda kutazama mechi ya kandanda katika kituo cha biashara kilicho karibu. Alirudi nyumbani mwendo wa saa tatu usiku. Mama yake alimletea chakula cha jioni lakini hakukila akisema kwamab hakuwa anahisi vyema. Kwa hivyo, aliingia nyumbani kwake na kulala, ripoti ilisoma.

Baada ya usiku huo mrefu, siku iliyofuatwa Okello alipatikana amefariki kwenye kitanda chake ambapo hakupatikana na majeraha yoyote.

Ushabiki wa kandanda ya Uingereza umekuwa ukiongezeka kwa kasi nchini Uganda ambapo mnamo Januari, tuliripoti kwamba mashabiki kadhaa wa timu ya Arsenal walitiwa mbaroni katika jiji la Jinja baada ya kuweka gwarida la kujitangazia ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza.