Mvulana wa kidato cha pili auawa siku chache baada ya kushinda 200K bahati nasibu

mvulana huyo wa miaka 17 alipatikana macho yake yalmeng'olewa, mkono wake wa kulia kuvunjwa na kulikuwa na majeraha kichwani.

Muhtasari

• Mvulana huyo alisemekana kushinda bahati nasibu baada ya kubashiri sahihi katika mechi ya fainali ya Carabao Man U dhidi ya Newcastle.

crime scene
crime scene

Biwi la simanzi liligubika kijiji kimoja kaunti ya Kitui baada ya mvulana mmoja mwanafunzi wa kidato cha pili kudaiwa kuuawa siku chache baada ya kushinda laki mbili taslimu pesa za Kenya, katika mchezo wa bahati nasibu.

“Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 17 alipatikana ameuawa na mwili wake kutupwa kwenye kichaka kilomita chache kutoka nyumbani kwake kijijini eneo la Maliku wilayani Katulani. Alikuwa amepotea kwa siku kadhaa,” jarida moja lilisema.

Kulingana na taarifa, mvulana huyo alikuwa ameshinda ‘bet’ ya laki mbili wiki mbili zilizopita baada ya kubashiri sahihi matokeo katika mechi ya fainali ya kombe la Carabao baina ya Manchester United na Newcastle United.

Mvulana huyo alitumia kitambulisho cha jirani yake kuandikisha laini ya simu ambayo alikuwa anatumia na simu kushiriki michezo ya bahati nasibu mitandaoni na siku hiyo, bahati ilisimama utosini mwake na kushinda laki mbili.

Baada ya kushinda pesa hizo kinyemela, hakumtaarifu mtu yeyote ila alimdokezea mama yake kwamba alitaka kuhamishiwa katika shule ya bweni akisema angeweza kujilipia karo, bila kufafanua njia ambazo angezitumia kulipa hiyo karo.

Jumatatu ya Februari 27 aliondoka nyumbani kwenda shuleni kama kawaida yake lakini hakurejea nyumbani jioni ya siku hiyo.

Familia ilimsubiri hadi siku ya pili ambapo pia alikosa kurejea nyumbani na walipofika shuleni waliambiwa kwamba hajakuwa shuleni katika sku hizo mbili ambazo alikosekana nyumbani.

Mwili wake, ukiwa umetolewa macho, uligunduliwa kwenye kichaka siku sita baada ya kuonekana mara ya mwisho - Jumamosi, Machi 4.

Mahali ambapo mwili wake ulipatikana ulikuwa na reli za matairi ya pikipiki, ikiashiria kuwa huenda aliuawa mahali pengine na mwili wake kupelekwa mahali kwenye pikipiki, jarida hilo liliripoti.

Uchunguzi wa upasuaji wa maiti uliofanywa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kitui ulifichua kuwa macho yake yalitolewa, mkono wake wa kulia ulikuwa umevunjika na kulikuwa na majeraha kichwani.