Sifuna:Serikali ilipuuza mialiko yetu ya mazungumzo

Seneta Sifuna alidai kuwa Azimio imekuwa ikifanya juhudi za kushirikisha serikali kujadili maswala muhimu

Muhtasari
  • "Dirisha la mazungumzo limefungwa kwa sababu tulitarajia tungejadili masuala haya ndani ya muda ambao tulitoa."
Mgombea useneta wa Nairobi kwa tiketi ya ODM Edwin Sifuna
Image: TWITTER// EDWIN SIFUNA

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amedai kuwa kupuuza ombi la Azimio la Umoja la kutaka kufanya mazungumzo na serikali ndio sababu ya maandamano makali dhidi ya serikali.

Seneta Sifuna alidai kuwa Azimio imekuwa ikifanya juhudi za kushirikisha serikali kujadili maswala muhimu yanayowasumbua Wakenya ikiwa ni pamoja na gharama ya maisha.

Akiongea kwenye kipindi cha Daybreak cha Citizen siku ya Alhamisi, Sifuna alibaini kuwa Azimio ililazimika kuanza kuandamana dhidi ya serikali, kwani katiba inatoa njia kama hiyo.

"Kulikuwa na maswala fulani ambayo tulihisi ni muhimu na utawala ungeshughulikia, moja ni ukweli kwamba Wakenya wanaendelea kuhisi gharama ya juu ya maisha swali la ni lini gharama ya unga itashuka limekuwa lengo kuu, " alisema Sifuna.

Aliongeza:

"Kwa bahati mbaya ndugu zetu wa upande wa pili wamepuuza mialiko yetu ya mazungumzo na tumebakiwa hatuna la kufanya zaidi ya kueleza masikitiko yetu kupitia kile ambacho katiba yetu imeturuhusu kutumia."

"Dirisha la mazungumzo limefungwa kwa sababu tulitarajia tungejadili masuala haya ndani ya muda ambao tulitoa."

Aliendelea kuongeza kuwa maandamano ya kitaifa, yanayoongozwa na mkuu wa Azimio Raila Odinga, kwa bahati mbaya imetajwa kuwa maandamano ya vurugu.

Sifuna alidai kuwa hakujawa na ripoti za uporaji au mapigano wakati wa maandamano na kwamba wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Kenya.