Mwanamume amchoma kisu mke wake, kisha amuamsha binti yao kuona alichokifanya!

Mwanamume huyo mhudumu wa bodoaboda alimchoma kisu mkewe na kumuua kisha akaamsha binti yao aliyemaliza kidato cha nne kuona.

Muhtasari

• Video iliyosambazwa kutokana na tukio hilo ilionyesha binti mdogo akilia sana huku akiliita jina la mama yake aliyefariki.

Kisu cha mauaji
Kisu cha mauaji
Image: Hisani

Wakaazi wa Kasarani katika kaunti ya Nairobi walipigwa na butwaa baada ya mwanabodaboda mmoja eneo hilo kumuua mke wake usiku na kisha kumuamsha binti yake kuona kitendo alichomfanyia mama yake.

Kulingana na taarifa iliyopeperushwa na runinga ya Kameme, mwanamume huyo mhudumu wa Boda Boda alimuua mkewe kwa kumchoma kisu mara kadhaa kabla ya kujaribu pia kujitoa uhai lakini hakufanikiwa.

Jirani aliyezungumza na waandishi wa habari alisema muuaji huyo alimwamsha bintiye ambaye ndiyo kwanza amemaliza kidato cha nne na aliyekuwa sebuleni na kumwambia aende kuona kuwa amemuua mama yao.

“Akamwambia binti yake ‘amka uone nimemfanyia nini mama yako’ binti huyo alipomuona baba yake akiwa na kisu kikiwa kimepakwa damu alimsihi asimdhuru, akaenda chumbani na kumkuta mama yake tayari amekufa na kando yake kulikuwa na dadake mdogo na akamchukua," jirani huyo aliambia Kameme TV.

Mwanamume huyo alijaribu kujimaliza, lakini binti huyo jasiri alifaulu kutuma ujumbe kwa marafiki wa mama yake, ambao walizua hofu. Mwanamume huyo alikuwa amejaribu kujidhuru, lakini polisi walifika kwa wakati ili kumzuia. Pia waliuchukua mwili. Video iliyosambazwa kutokana na tukio hilo ilionyesha binti mdogo akilia sana huku akiliita jina la mama yake aliyefariki.