Maandamano yatafanyika kila Jumatatu - Raila Odinga

Odinga alisema maandamano hayo yatafanyika kila Jumatatu mpaka pale Ruto atakaposikiliza matakwa yao.

Muhtasari

• Katika msafara huo, Odinga aliandamana na wanachama wengine akiwemo Kalonzo Musyoka, Martha Karua na Eugene Wamalwa.

Image: Facebook

Kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ametangaza wazi kwamba maandamano dhidi ya serikali ya rais William Ruto yatakuwa yakifanyika kila Jumatatu mpaka wakati matakwa yao yatakaposikilizwa na serikali ya rais Ruto.

Odinga alizungumza katika mtaa wa Eastleigh Nairobi ambako msafara wake ulielekea baada ya kuzuiliwa kuingia maeneo ya katikati mwa jiji na maafisa wa polisi ambao waliwatupia vitoa machozi.

Odinga alisema kwamba wana matakwa matatu ambayo wanataka serikali ya Ruto kutii ikiwemo kufunguliwa kwa seva za tume ya uchaguzi na mipaka IEBC, kupunguzwa kwa gharama ya maisha na kusitishwa kwa shughuli ya kuwateua makamishna wa IEBC - shughuli ambayo inasimamiwa na rais Ruto.

Odinga alisema kwamba shughuli hiyo ya kuwateua makamishna hao inafaa kuwajumuisha watu kutoka mirengo yote na wala sio mrengo wa serikali.

Katika msafara huo, Odinga aliandamana na wanachama wengine akiwemo Kalonzo Musyoka, Martha Karua na Eugene Wamalwa.

Msafara huo ulitafuta njia mbadala baada ya kuzuiliwa kuingia katikati mwa jiji kutoka barabara ya Kenyatta ambapo walizunguka jiji na kuingia Kamukunji ambapo Odinga aliwahutubia wafuasi wake kwa muda mfupi kabla ya kuelekea maeneo ya Pangani kuingia Eastleigh.

Kalonzo alipokuwa anazungumza, polisi walirusha vitoa machozi na kusambaratisha hotuba yake ambapo msafara huo ulilazimika kuondoka na kwendelea na ziara yao katika mtaa huo.