Mwili wafukuliwa baada ya mwezi na kukutwa umegeuzwa ukiwa bila sanda!

Wanakijiji waliona dalili za kaburi kuhitilafiwa na kutaka kibali kutoka kwa mamlaka kuufukua mwili huo.

Muhtasari

• Baada ya kufukuliwa kwa kaburi, mtoto huyo alipatikana lakini hakukuwa na sanda na mwili wake ulikuwa umegeuzwa.

• Wakaazi hao walisema vitendo vya watu kupatikana na viungo vya mwili si jambo geni katika eneo hilo.

Mwili wafukuliwa na kuutwa umegeuzwa.
Mwili wafukuliwa na kuutwa umegeuzwa.
Image: Screengrab

Familia moja imepigwa na butwaa baada ya kufukua kaburi la mpendwa wao na kukuta mwili umegeuzwa kinyume na walivyousitiri awali wakati wa maziko.

Tukio hilo lilijiri katika mkoa wa Geita nchini Tanzania ambapo baada ya malalamishi kutoka kwa wanafamilia ambao walidai kwamab kaburi la mpendwa wao mtoto lilikuwa na ishara ya kuhitilafiwa, walitaka kibali ili kufukua na kuhakikisha iwapo mwili huo upo kaburini au umeibwa.

Mtoto huyo marehemu alizikwa mwezi uliopita lakini baada ya siku chache, familia ikazua madai kwamba kaburi hilo lilionekana kuhitilafiwa na wikendi iliyopita baada ya mamlaka husika kutoa kibali cha kufukuliwa kwa hakiisho, wanafamilia kwa kushirikiana na mamlaka walianzisha shughuli ya kuufukua mwili wake.

Baada ya kuufukua, waliukuta mwili huo ukiwa ndani ya jeneza kama ambavyo waliusitiri hapo awali lakini butwaa waliyokumbana nayo ni kwamba mwili huo ulikuwa umegeuzwa, kulingana na wale waliousitiri kipindi cha kumpa buriani.

“Baada ya kwamab tumefungua lile jeneza, tulikuta mwili umo lakini umegeuzwa. Lakini sanda hatukuiona. Sanda hatukuiona kwa uzuri, tuliona mwili umo, kichwa kimo na viungo vingine vimo. Lakini ni jambo ambalo limekuwa likitishia Amani sana,” Lucas Madaha ,mmoja wa wanafamilia waliokuwa katika kuuandaa mwili huo na sambamba katika kuufukua alisema.

Wakaazi hao walisema tukio la kuukuta mwili umegeuzwa liliwapiga butwaa pakubwa kwani hawajui kilichotokea kufuatia wasiwasi wa Imani za kishirikina zilizotokea katika kaburi la mtoto huyo.

Wakaazi hao walisema vitendo vya watu kupatikana na viungo vya mwili si jambo geni katika eneo hilo.