Nimesema hakuna maandamano Lang'ata! - Jalang'o amwambia Raila Odinga

Jalang'o alisisitiza kwamba haja yake kuu ni kushirikiana na serikali kuleta maendeleo katika eneo bunge lake, jambo ambalo maandamano hayatataua.

Muhtasari

• "“Ni lazima tuwe kama mifano bora katika kujibeba kwetu na pia katika Imani, katika mapenzi na katika utoaji wa huduma" - Jalang'o

Jalang'o amwambia Odinga hakuna maandamnao Lang'ata
Jalang'o amwambia Odinga hakuna maandamnao Lang'ata
Image: Facebook

Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o ameendeleza ukaidi dhidi ya kiongozi wake wa chama, Raila Odinga kwa kupinga vikali wito wake wa kuwataka wanachama wote wanaoegemea mrengo wa upinzani kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya maandamano.

Jalang’o ambaye alikuwa anazungumza katika ibada moja ya kanisa Jumapili alisisitiza kwamba anachokiweka mbele kwa wakati huu ni kuboresha huduma kwa watu wa eneo bunge lake la Lang’ata na wala hakutakuwa na nafasi yoyote au muda wa kuharibu katika kushiriki maandamano kama ilivyotakiwa na kiongozi wake wa chama.

“Ni lazima tuwe kama mifano bora katika kujibeba kwetu na pia katika Imani, katika mapenzi na katika utoaji wa huduma. Kesho kuna maandamano si ndio? Mimi Lang’ata nimesema hakuna maandamano kesho. Hiyo haitabadilisha urafiki wetu, kama unaunga mkono maandamano amka mapema ufike huko mapema lakini hapa Lang’ata hakutakuwa na maandamano,” Mbunge huyo wa ODM alisema.

Mbunge huyo mkaidi wa maagizo ya chama alisisitiza kwamba wanataka kushirikiana na serikali kwa ukaribu ili kuleta maendeleo katika eneo bunge lake.

Wikendi kulikuwa na klipu ambayo ilikuwa inasambazwa mitanaoni ikimuonesha Jalang’o akitoa sababu zake kwa nini aliamua kushirikiana na serikali ya Ruto licha ya kupata pingamizi kali kutoka kwa viongozi wa upinzani.

Jalang’o pia alifutilia mbali uwezekano wa kinara wa ODM Raila Odinga kuwa rais mbele yake, akisema kuwa atakuwa mtu wa kwanza kutoka Luo Nyanza kuwa rais wa Kenya.

Alisema ziara yake ya kujinyenyekeza kwa rais Ruto ni njia moja ya kujifunza filosofia ya kisiasa kutoka kwa kiongozi huyo wa taifa ambaye Jalang’o alimtaja kama mwanasiasa ambaye hajawahi shindwa katika uchaguzi wowote.