Wakili Ombeta atetea wanandoa walioonekana wakiingiza kondoo ndani ya gari kwa Uhuru

"Hawa si wezi, wanajaribu kumuokoa kondoo aliyekuwa amekwama," Ombeta alisema.

Muhtasari

• Ombeta alisema kwamba wanandoa hao si wizi walikuwa wanafanya bali ni uokozi walikuwa wanatoa kwa kondoo huyo aliyekuwa akirandaranda barabarani.

Ombeta atetea wanandoa walionekana wakiingiza kondoo kwa gari
Ombeta atetea wanandoa walionekana wakiingiza kondoo kwa gari
Image: Twitter

Jumatatu wakati wa maandamano ya muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya, mali yaliharibiwa katika sehemu mbali mbali na waandamanaji waliogeuka kuwa wahuni.

Baadhi ya watu walionekana kulivamia shamba la rais mstaafu Uhuru Kenyatta huko Ruiru, Northgates na kukata miti, kuiba mifugo wa idadi isiyokadirika pamoja pia na kuchoma eneo hilo.

Mitandaon, kumekuwa na picha zikiwaonesha wavamizi hao wakiendesha shughuli za uvamizi, wengi wakionekana kuondoka na kondoo kwa kuwabeba mabegani, wengine wakishirikiana kubeba kama mizigo na wengine wakipakia kondoo hao ndani ya magari yao.

Katika moja ya picha ambazo zimezua mjadala mkali mitandaoni, mwanamume mmoja na mwanamke anayedhaniwa kuwa mpenzi wake walionekana pia wakishirikiana kwa wepesi kumuingiza kondoo mmoja ndani ya buti la gari lao dogo.

Picha hiyo ambayo ilipakiwa na wakili Donald Kipkori, aliwataka wanandoa hao kwa majina akihoji kutaka kujua ni nini watawaambia watoto wao walimtoa kondoo wapi.

“Baada ya kuiba mbuzi kutoka Northlands ya Kenyatta, Je Kamarah Pitah na mkewe watawaambia watoto wao nini? Watasema nini wakienda kanisani Jumapili? Picha hii itawasumbua milele. Mbuzi mmoja akighairi maisha yako milele,” Kipkorir alisema.

Hata hivyo, wakili mwenzake, Cliff Ombeta alijitokeza kwa wepesi mno akiwatetea wanandoa hao katika kile alisema kwamba huo si wizi bali walikuwa wanajaribu kumpa huduma za uokozi kwani alikuwa amepotea kutoka kundini.

“Huu sio wizi. Wanamwokoa kondoo aliyekwama ambaye alikuwa akirandaranda kwenye barabara hatari na yenye shughuli nyingi. Kusema ukweli walikuwa wamemuacha tu salama,” Ombeta alitetea.

Wakili Ombeta ambaye alijaribu bahati yake katika kiti cha ubunge Bonchari bila mafanikio katika uchaguzi uliopita amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa miaka mingi akitetea watuhumiwa wa kesi mbalimbali zenye ukakasi.