Jamaa aishtaki kampuni ya kamari kwa kukosa kumpa 500K alizoshinda kwa bet ya Ksh 10!

Juma alisema utabiri wake wa mechi 8 ulitimia lakini kampuni ya kamari ikabadilisha matokeo ya timu moja kwenye wavuti wao.

Muhtasari

• Juma na kaka yake Collins Kizito waliweka dau la bahati nasibu la Sh500,000 kwenye jackpot ya Sababisha ya michezo 8 na Sh10 mnamo 18 Februari.

• Kulingana na Bw Juma, utabiri wote ulitimia, na wakasubiri kuchukua pesa zao za zawadi.

Pesa za Kenya
Pesa za Kenya
Image: HISANI

Mwanamume mmoja kutoka kaunti ya Nakuru ameishtaki kampuni moja ya Kamari nchini kwa kukataa kumlipa pesa Zaidi ya nusu milioni za Kenya alizoshinda kutoka kwa bet ya shilingi kumi.

Kulingana na jarida la Nation, Bw David Juma, mcheza kamari anayeishi Nakuru ambaye alishinda jackpot ya Sh500,000 baada ya kuweka dau la Sh10 kwenye jukwaa la ****, ameishtaki kampuni hiyo kwa kukataa kulipa madai yake.

Juma na kaka yake Collins Kizito waliweka dau la bahati nasibu la Sh500,000 kwenye jackpot ya Sababisha ya michezo 8 na Sh10 mnamo 18 Februari.

Kulingana na Bw Juma, utabiri wote ulitimia, na wakasubiri kuchukua pesa zao za zawadi.

Hata hivyo, walishtuka walipoingia kwenye tovuti hiyo na kugundua kuwa kampuni hiyo ilionyesha kimakosa kuwa mechi moja haikutabiriwa kwa usahihi.

Waliamua kuwasiliana na kampuni hiyo ili kujaribu kurekebisha hitilafu hiyo, lakini jitihada zao ziliambulia patupu.

Mchezaji huyo alilalamika kwamba alitumia wakati, pesa na nguvu kuchambua michezo hiyo na kusalitiwa na kampuni iliyomwangusha.

Katika kesi yake katika Mahakama ya Madai madogo ya Nakuru, Bw Juma alishtaki Shop and Deliver Limited, kampuni inayofanya biashara ya kampuni hiyo ya kamari.

Katika ushahidi wake, aliambatanisha hati za kamari na jumbe za miamala pamoja na matokeo ya mechi kwenye ombi hilo.

Bw Juma anadai kuwa vitendo vya kampuni hiyo vilikuwa vya nia mbaya na kukiuka kandarasi.