Azimio washutumu DP Gachagua, waziri Kuria kwa kuajiri wahuni kutatiza maandamano

"Hao ndio wanaambiwa wavamie nyumba ya viongozi wao na kushambulia watu na mali katika maeneo tofauti ya Nairobi."

Muhtasari
  • "Wale vijana walikuwa Northlands ndio walikuja Jubilee makao makuu."
Azimio washutumu DP Gachagua, waziri Kuria kwa kuajiri wahuni kutatiza maandamano
Image: TWITTER/RAILA ODINGA

Uongozi wa chama cha muungano cha Azimio la Umoja One Kenya umewashutumu Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Biashara Moses Kuria kwa  kuajiri wahuni wanaodaiwa kusababisha fujo wakati wa maandamano ya upinzani dhidi ya serikali.

Akizungumza wakati wa wanahabari Jumanne, kinara mwenza wa Azimio na kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua alidai kuwa viongozi watano wa Kenya Kwanza kutoka eneo la Mlima Kenya wamekuwa wakiwaajiri vijana kutoka eneo hilo, kwa amri ya DP Gachagua, ili kutatiza maandamano ya Azimio.

"Ni vijana kutoka Kati mwa Kenya wanaotumiwa kupigana. Walitumiwa kuvamia shamba la Northlands na makao makuu ya Jubilee hivi majuzi," alisema Karua.

"Hao ndio wanaambiwa wavamie nyumba ya viongozi wao na kushambulia watu na mali katika maeneo tofauti ya Nairobi."

Matamshi ya Karua yaliungwa mkono na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ambaye alidai kuwa mpango wa kuwaajiri washukiwa hao uliandaliwa katika maeneo ya nyumbani kwa Waziri wa Biashara Kuria.

"Tarehe 26, mwezi wa tatu, viongozi walikutana kwa Moses Kuria. Kati ya hao viongozi Kimani Ichung'wa, Ndindi Nyoro, Kanini Kega na Sabina Chege walikua. Kiongozi wa kikosi hiki ni Rigathi Gachagua na wakapanga kuvamia shamba la Northlands, wakapanga kuvamia industrial complex ya Specter na wakavamia," alisema Kioni.

"Wale vijana walikuwa Northlands ndio walikuja Jubilee makao makuu."

Mnamo Aprili 30, Kioni kiliendelea, viongozi waliotajwa hapo juu wa Kenya Kwanza waliripotiwa kugusa eneo la Thika, Kaunti ya Kiambu, ambapo walidai kuwa wangewalinda watu wowote ambao 'wangeondoa' uongozi wa Azimio.

"Walisema ya kwamba wamekubali kutumia muda wao ambao umebaki wakiwa kortini kwa kesi mmoja wa viongozi wa Azimio ameuwawa. Yaani wanasema wauawe wao watakuwa kortini miaka yao yote wakitetea jambo hilo," alisema.

"Hii mkutano pia ilifanywa Kikuyu na vijana waliokuwa wanaongeleshwa ni wakikuyu. Leo kuna ghasia ambazo zimetokea; sisi wana-Azimio hatukuenda kule. Huo uliotokea ni wale vijana ambao walikubali."