Polisi nchini Uganda wameanzisha uchunguzi na msako dhidi ya kisa ambapo mwanamke mmoja anadaiwa kumdunga sindano yenye sumu mke mwenza ya kuchimba mitini kusikojulikana.
Kulingana na jarida la Nile Post nchini humo, Tukio hilo lililotokea eneo liitwalo Kyotera na lilimshuhudia Jackie Namubiru akimvamia mke mwenza Nakimera Lydia mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni mmiliki wa saluni.
Msemaji wa jshi la polisi nchini humo Fred Enanga alinukuliwa na jarida hilo akisema kwamba walipokea ripoti kuwa Namubiru alitoroka baada ya kumvamia mke mwenza kwa sindano yenye sumu.
“Mshukiwa alimdunga mwathiriwa sindano, iliyokuwa na vitu vinavyoshukiwa kuwa vya sumu. Alikimbizwa katika zahanati ya Bulamu, na baadaye alihamishiwa kliniki ya Byansi katika Jiji la Masaka akiwa katika hali mbaya. Mwathiriwa alifariki kutokana na sumu hiyo mnamo tarehe 23.04.2023 mwendo wa saa kumi na mbili na nusu jioni,” msemaji wa polisi, Fred Enanga alisema Jumanne.
Msemaji wa polisi alilaani kitendo hiki cha unyanyasaji cha Namubiru dhidi ya mke mwenza.
"Tabia za wivu zinaweza kuharibu kama ilivyo katika kipengele hiki, lakini vitengo vya ulinzi wa familia vina mbinu mbadala ya kutatua migogoro ya familia. Msako mkali wa kumtafuta mshukiwa unaendelea,” Enanga alibainisha.
Kisa hiki kinaripotiwa kwenye vyombo vya habari siku moja tu baada ya tukio jingine la kukata maini ambapo waziri wa leba nchini humo anadaiwa kushambuliwa na mlinzi wake.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, waziri huyo alishambuliwa na mlinzi wake nyumbani kwake ambaye alimfyatulia risasi Zaidi ya mara ishirini kabla ya kujigeuzia mtutu wa bunduki na kujipiga risasi pia.