Waanike maafisa wa polisi waliokuteka nyara-Boniface Mwangi kwa Itumbi

Polisi hata hivyo walikanusha kufahamu madai hayo.

Muhtasari
  • Mnamo Desemba 2021, Itumbi alitekwa nyara alipokuwa akitoka kwenye kinyozi huko Thindigua, Kiambu.
Image: FACEBOOK// DENNIS ITUMBI

Mwanaharakati Boniface Mwangi amemtaka katibu mkuu wa utawala wa ICT Dennis Itumbi kuwataja maafisa wa polisi waliomteka nyara na kumshambulia mwaka wa 2021.

Alisema kwa kuwa Itumbi sasa alikuwa mtumishi wa umma, sasa anaweza kuweka majina yao hadharani na kutoa taarifa ya mwenendo wa kesi hiyo.

"Hey @OleItumbi, kwa kuwa sasa uko serikalini, unaweza kuweka hadharani majina ya maafisa wa polisi waliokuteka nyara, kwa maagizo ya nani na kuwawajibisha?" Aliuliza.

Kuwawajibisha wale waliomtesa aliyekuwa Mtaalamu wa Mbinu za Kidigitali Mwangi alisema, utakuwa mwanzo mzuri wa kukomesha ukosefu wa haki unaosababishwa na polisi.

"Ikiwa tunataka kukomesha mauaji ya kiholela na utekaji nyara wa polisi, ni lazima waliohusika wawajibishwe," alisema.

Mnamo Desemba 2021, Itumbi alitekwa nyara alipokuwa akitoka kwenye kinyozi huko Thindigua, Kiambu.

Saa kadhaa baadaye, alipatikana na dereva wa teksi, akiwa uchi na akichechemea katika eneo la Lucky Summer karibu na uwanja wa Kasarani.

Alikuwa amevunjika miguu yote miwili na mkono wake wa kushoto na pia alikuwa na majeraha sehemu nyingi za mwili wake. Jicho lake la kushoto lilikuwa linavuja damu.

Kakake David alisema Itumbi aliwaambia watu waliomteka nyara na kumpiga walidai kuwa maafisa wa polisi.

Polisi hata hivyo walikanusha kufahamu madai hayo.

Aidha Itumbi alisema kwamba aliwasamehe waliomtendea unyama huo.

Boniface Makokha alimchukua Itumbi kutoka eneo ambalo alikuwa ametupwa mtaani Kasarani, akamfunika uchi kwa kitamaa na kumpatia soda kabla ya kumpeleka kupokea matibabu katika kituo cha afya kilichokuwa karibu.

Makokha alisimulia yaliyojiri usiku huo huku akieleza kwamba mwanzoni alipokuwa anasimamisha gari lake hakufahamu kuwa mhasiriwa alikuwa ni mtaalamu huyo wa masuala ya kidijitali.

“Nilikuwa naelekea nyumbani nilipomwona mtu mmoja ambaye alikuwa uchi akizungumza na waendesha bodaboda. Nilipokagua vizuri niliona ni mtu aliyekuwa kwenye shida nikajitolea kusaidia,” Makokha alisema.

Makokha alisema kwamba baada ya kugundua kuwa jamaa aliyesimama kuokoa ni Itumbi aliamua kuficha uchi wake kwanza kutokana na heshima kubwa aliyo nayo kwa mwanablogu huyo.