Rais Ruto, DP Gachagua wainuka na kunyenyekea wakimsalimia Raila Odinga

Odinga alifika katika hafla ya mazishi ya Mukami Kimathi ambapo aliwapata viongozi hao wameketi na walipomuona waliinuka na kumpa salamu huku wakinyenyekea.

Muhtasari

• Ruto na Gachagua walitangulia kufika katika hafla hiyo huko Nyandarua na Odinga alifika nyuma.

• Raila alimsalimia Naibu Rais Rigathi Gachagua na kumwendea Rais mashuhuri William Ruto.

• Ruto aliinuka kupeana naye mkono huku umati ukishangilia.

Ruto na Rigathi wainuka na kunyenyekea kumsalimia Raila Odinga katika mazishi ya Mukami Kimathi.
Ruto na Rigathi wainuka na kunyenyekea kumsalimia Raila Odinga katika mazishi ya Mukami Kimathi.
Image: PSC

Kwa mara ya kwanza rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachaua wamekutana uso kwa uso na 'mbaya' wao wa kisiasa Raila Odinga na kusalimiana naye hadharani.

Watatu hao walikutana katika hafla ya kumpa buriani marehemu Mukami Kimathi ambaye alikuwa mmoja wa wanachama wa Mau Mau - kundi la mashujaa waliopigania uhuru wa Kenya kutoka kwa wakoloni kati ya mwaka 1952 hadi 1963.

Ruto na Gachagua walitangulia kufika katika hafla hiyo huko Nyandarua na Odinga alifika nyuma na kuelekea kwenye jeneza la Mukami na kutoa heshima yake kwake.

Kisha akaendelea hadi kwa viongozi waliokuwepo.

Raila alimsalimia Naibu Rais Rigathi Gachagua na kumwendea Rais mashuhuri William Ruto.

Ruto aliinuka kupeana naye mkono huku umati ukishangilia.

Mazishi ya Mukami yalishuhudia Ruto na Raila wakikutana kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 uliokuwa na ushindani mkali.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Ruto, Gachagua na Raila kukutana ana kwa ana.

Viongozi hao wamekuwa wakirushiana vijembe hadharani kuhusu gharama ya maisha, Mswada wa Sheria ya Fedha, 2023, maandamano, sakata ya Shakahola, uteuzi wa serikali miongoni mwa masuala mengine.

Raila ni miongoni mwa viongozi wakuu walioshiriki ibada ya mazishi.

Raila alikuwa amethibitisha kuwa atahudhuria ibada ya mazishi.

“Siwezi kukosa mazishi ya Shujaa Mama Mukami wa Kimathi. Tumekuwa karibu sana na nitakuwa Njabini kwa sherehe yake ya mwisho duniani,” Raila alisema.

Mukami Kimathi alifariki akiwa na umri wa miaka 96 alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kupata matatizo ya kupumua.

Aliaga dunia Alhamisi usiku, Mei 4, 2023