DJ Brownskin akamatwa kwa siri kuhusiana na kifo cha mke wake

Anachunguzwa kuhusiana na kifo cha mkewe, Sharon Njeri, 24, aliyefariki kati ya usiku wa Julai 29 na Julai 30, 2022.

Muhtasari

•Maafisa wa DCI walimkamata Brownskin katika klabu maarufu ya Kasarani na kwa sasa yuko kizuizini katika kituo cha polisi cha Kasarani.

•Haya yanajiri baada ya polisi kupata kibali kutoka kwa mahakama ya Makadara kumshikilia kwa siku saba ili kukamilisha uchunguzi.

DJ Brownskin
Image: HISANI

Taarifa zinazotufikia ni kwamba mcheza santuri Michael Njiiri almaarufu Dj Brownskin alikamatwa siku ya Madaraka Dei, Juni 1, 2023.

Wapelelezi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walimkamata Brownskin katika klabu maarufu ya Kasarani na kwa sasa yuko kizuizini katika kituo cha polisi cha Kasarani.

Haya yanajiri baada ya polisi kupata kibali kutoka kwa mahakama ya Makadara kumshikilia kwa siku saba ili kukamilisha uchunguzi.

Anachunguzwa kuhusiana na kifo cha mkewe, Sharon Njeri, 24, aliyefariki kati ya usiku wa Julai 29 na Julai 30, 2022.

Hii ni kuhusiana na video ambayo ilisambaa kama moto wa nyika mwanzoni mwa mwaka huu ambapo DJ huyo alionekana akimhimiza marehemu mkewe Sharon kujitoa uhai.

Katika video hiyo, mwanamume mmoja nyuma ya kamera anasikika akimuomba marehemu Sharon Njeri aendelee na kuchanganya sumu.

Sharon alionekana akiendelea kufanya hivyo kwa hiari na hatimaye kumeza sumu hiyo wakati mwanamume akiendelea kurekodi. Ndani ya muda mfupi mwanamke huyo alionekana akikunjamana kwa maumivu kabla ya kila kitu kutulia.

Mwanamume aliyekuwa akirekodi anadaiwa kuwa DJ Brownskin ambaye alikuwa na watoto wawili na marehemu Sharon. Ingawa alijitoa uhai mnamo Julai 2022, haijulikani wazi sababu ya video hiyo kutolewa mwaka huu.

Ingawa hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya DJ Brownskin wakati huo, wakili maarufu Danstan Omari alitoa maoni kwamba inawezekana kumshtaki DJ huyo kwa kosa la jinai.

Omari alisema kuwa mtu yeyote anayeona mtu akijitoa uhai na kushindwa kuchukua hatua yoyote ya kumsimamisha au kuripoti ana hatia ya kosa chini ya Kanuni ya Adhabu kifungu cha 225 (Kusaidia kujiua).

Brownskin mwenyewe alifunguka kuhusu video hiyo mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu akisema,

"Mtu yeyote anayeamini uwongo kukuhusu kabla ya kusikia upande wako wa hadithi alikuwa tayari anatafuta njia ya kuwa dhidi yako," ilisoma nukuu iliyoshirikiwa na Brownskin.