Mwanamume ashtakiwa kwa kujaribu kumbaka baby mama wake

Alishtakiwa kwa kosa la pili la kufanya kitendo kichafu na mtu mzima kinyume na sheria ya Kenya.

Muhtasari

•AR alishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Kibera Ann Mwangi ambapo alikanusha mashtaka hayo.

•Mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa hawezi kugura nchini na akaiomba mahakama kumwachilia kwa bondi.

Mahakama ya Kibera.
Mahakama ya Kibera.
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanaume mmoja mnamo Jumatatu alifunguliwa mashtaka kwa madai ya kujaribu kumbaka mwanamke ambaye anaaminika kuwa na mtoto pamoja naye.

AR alishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Kibera Ann Mwangi ambapo alikanusha mashtaka hayo.

Mahakama ilisikia kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Machi 28, 2023, katika mtaa wa Uthiru, kaunti ndogo ya Dagoreti ndani ya Kaunti ya Nairobi.

Alishtakiwa kwa kosa la pili la kufanya kitendo kichafu na mtu mzima kinyume na sheria ya Kenya.

Kupitia kwa wakili wake, mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa hawezi kugura nchini na akaiomba mahakama kumwachilia kwa bondi.

Pia aliitaka mahakama kumpa ushahidi wote wa maandishi ambao upande wa mashtaka ulinuia kuutegemea wakati wa kesi hiyo.

Wakili wa mshtakiwa pia aliambia mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa na uwezo wa kulipa dhamana ya pesa taslimu 50,000 pekee yake.

Mahakama ilimwachilia kwa bondi ya shilingi 200,000 na dhamana mbadala ya pesa taslimu 50,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Hakimu aliamuru kesi hiyo isikilizwe Juni 12 kwa ajili ya maelekezo zaidi kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa rasmi.